*Ni kutekeleza agizo la Waziri Mkuu
Na Renatha Kipaka, Bukoba
Siku chache baada ya kutokea ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air mjini Bukoba na kuua watu 19 na majeruhi 24, baadhi ya wavuvi walioshiriki katika uokozi wamepigwa msasa.
Wavuvi hao ni kutoka katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na wengine nikutoka Katika wilaya ya Misenyi ambao idadi yao ni 60.
Mafunzo hayo yametolewa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kujenga uwezo wa vikundi vya wavuvi walioshiriki katika shughuli ya uokoaji.
Wakizungumza na Mtanzania Digital Novemba 28, mwaka huu mjini Bukoba mara baada ya mafunzohayo kwa vitendo wakiwa wamevalia maboya na baadhi ya vifaa vya kushika ndani ya Ziwa Victoria wamesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawasaidia kukabiliana na majanga.
Mkazi wa Nyamkazi, Beatus Mweyaga Mvuvi amesema, awali amekuwa anaogelea akiwa amevaa mavazi yake ya kawaida ambayo siyo salama sana ikilinganishwa na lifejacketi.
Mweyanga amesema kuna wakati majanga yamekuwa yakitokea lakini inashindikana kuokoa sababu ya umbali wa eneo na hakuna vifaa vyenye kumfikisha na kusaidia mhanga.
Kwa upande wake, Justine Goston ambaye pia ni mvuvi amesema, mafunzo hayo yamekuwa sehemu ya kuwaongezea umakini na usalama pindi wanapokuwa kwenye shughuli zao na hata nyakati za uokozi.
“Kabla ya kuokoa mtu inatakiwa kwanza nijiokoe mimi na lazima nijue usalama wangu uko wapi na mazingira niliyopo yakoje kwanza itanisaidia mimi kufanya uokoaji,”amesema Goston.
Mkazi wa Wilaya ya Misenyi, Harid Musa amesema, asilimia kubwa watu hutumia usafiri wa mitumbwi kwenda kwenye visiwa kutafuta riziki zao lakini walio wengi hawana ujuzi kamili kuhusiana na uokoaji.
“Hivi vifaa vitatupa wepesi wa kukimbia kwa haraka na kusaidia wengine ambao wamepatwa na ajali, tofauti na hapo awali lazima utumie mtumbwi,” amesema Mussa.
Upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila amesema eneo kubwa la ziwa Victoria takribani asilimia 40 lipo upande wa mkoa wa Kagera ambapo kuna visiwa 32 na kata tano zenye watu 1,050 ambao maisha yao hutegemea safari za maji.
“Vifaa vinavotumika zaidi ni boti na mitumbwi kwenda kufanya uvuvi, visiwa 37 vinakaliwa na watu ikiwa visiwa vitano viko wilaya ya Muleba na viwili viko Manispaa ya Bukoba na usafiri wa maisha ya watu hao sio salama sana,” amesema Nguvila.
Mkurugenzi Msaidizi wa Maafa, Luten Kanali Selestine Masalamado amesema, ofisi ya Waziri mkuu kupitia kitengo cha maafa imeona umuhimu wa vikundi vya wavuvi kwa kuwa na mchango mkubwa kwenye maokozi pindi majanga yanapotokea.
“Hivyo, sasa kuanzishwa vikundi kwenye maziwa makuu na ukanda wa bahari kupitia makundi haya ya wavuvi kuwapa elimu ambayo na wao wataipata kwa wengine lengo ni kujenga uwezo pamoja na kufanya maokozi ya maafa na majanga yanayoweza kutokea,” amesema Masalamado.