Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Rais Samia Suluhu Hassan amepokea na kuridhia upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wa umma 116,000 nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa wakati akizungumza na Wafanyakazi wa Kampuni ya Nyumba ya Watumishi Housing (WHC) Jumatatu Juni 28, 2021.
“Lazima tukumbuke kwamba rais ndiye mfariji namba moja, ndiyo maana mpaka kufikia jana (Juzi) saa nane Mchana Rais Samia Suluhu amepokea na kuridhia upandishwaji wa madaraja ya watumishi wa umma zaidi ya 116,000.
“Hivyo hiyo ina maana kwamba mishahara yao imepanda, kwani ofisi yangu ilimuomba zaidi ya Sh bilioni 300 ambazo amezitoa.
“Fedha hizi zinakwenda kufanya nyongeza ya mkishahara kwa watumishi ambao wamepandishwa madaraja.
“Mama ameamua kutupandisha madaraja kwa watumishi ambao walikuwa hawajapandishwa kwa zaidi ya miaka sita, kwani kikatiba yeye ndiye mtendaji mkuu na mfariji namba moja wan chi.
“Na ofisi yangu tunategemea kumuomba zaidi pengine mwezi ujao aridhie watumishi wengine waliobaki, kwani kuna baadhi ya taasisi na Halmashauri ambao wamechelewa kutuletea taarifa ambapo nitachukua hatua kwa wakurugenzi wote na kwa maafisa utumishi ambao wamechelewa kutuletea taarufa kwa kuwaondosha kwenye nafasi zao sababu wanawanyima haki watumishi, kwani dhamira ya rais ni kuona hakuna mtu ambaye haki yake inachelewa, hivyo haki ya mtumishi haitaombwa jambo la msingi ni lazima watumishi tuwe tayari kuwajibika hasa kwa watumishi wa chini,” amesema Mchengerwa.
Ameongeza kuwa kuna watanzania takribani milioni 60 ambao wengi wao wanauwezo mkubwa pengine zaidi ya watumishi walipo kazini na wanatamani sana kufanya kazi serikalini sababu tumerejesha hadhi.
“Ukiwa mtumishi wa umma wewe unakuwa kama dhahabu, ndiyo maana rais anahakikisha haki zenu zinazingatiwa.
“Wapo watumishi ambao waliowahi ambao wataaza kuona mabadiliko kwenye mshahara wa mwezi huu na waliochelewa wataona kwenye mshahara wa mwezi ujao,” amesema Mchengerwa.
Kuhusu malimbikizo ya mishahara, Mchengerwa amesema tayari madeni hayo yamelipwa.
“Hata wale ambao walikuwa na malimbikizo mbalimbali ya mishahra ofisi yangu tayari imelipa malimbikizo ya watumishi karibu 12, 000 ambao walikuwa na haki zao za malimbikizo mbalimbali,” amesema Mchengerwa.