SANAA, YEMEN
SHIRIKA la Kimataifa la Misaada kwa watoto, Save the Children limesema watoto wasiopungua 85,000 walio chini ya umri wa miaka mitano huenda walifariki dunia kutokana na njaa na maradhi tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen mwaka 2015.
Save the Children limesema kiwango cha makadirio hayo kinatokana na idadi ya wastani ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mbaya.
Umoja wa Mataifa (UN) umesema umewaathiri watoto zaidi ya milioni 1.3 tangu muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia ulipojiingiza kwenye vita nchini Yemen dhidi ya waasi wa Kihouthi Machi 2015.
Mkurugenzi wa Save the Children nchini Yemen, Tamer Kirolos amesema wakati kukiwa na watoto wanaouawa kwenye mashambulizi ya mabomu pia wengine wengi wanaokufa kutokana na njaa licha ya kuwa hilo linaweza kuzuilika.
Vita hivyo pamoja na mzingiro unaoongozwa na Saudi Arabia vimesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambao haujawahi kuonekana duniani.