Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, amewataka Watanzania kujitokeze kwa wingi kwenye nyanja hiyo sababu ndani ya bahari kuna fursa nyingi na kuzichangamkia.
Hayo yamebainishwa leo Juni 27, jijini Dar es Salaam na Waziri huyo wakati akifungua kongamano la pili la Uchumi wa Bluu liloandaliwa na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).
“Ndani ya bahari kuna rasilimali nyingi zinazoonekana kwa macho na zisizoonekana, Kuna mafuta na gesi, hizo zote ni fursa ya uchumi wa bluu, Watanzania zichangamkieni,” amsema Makame.
Amefafanua kuwa fursa zinazopatikana kupitia uchumi wa bluu, zimewafanya Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuvalia njuga kutangaza fursa hizo.
Amesema uchumi wa bluu ni mwarobaini wa umaskini wa Watanzania, kwani asilimia 75 ya usafirishaji wa karibu vitu vyote tunavyoviona vimesafirishwa kwa njia ya bahari.
Aidha amesema ni muhimu kuthamini mchango wa mabaharia na pia kuhimiza Watanzania wengi zaidi kusomea gani hiyo.
Nae Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (MDI), Dk. Tumaini Gurumo amesema chuo hicho kina mipango kuhamasisha Watanzania kusomea ubaharia na masomo mengine yanayohusiana na mambo ya baharini.
“Kwa mfano tumejiwekea malengo ya miaka mitano, kufikia mwaka 2026 tuwe na wanafunzi 26,000 wa fani mbalimbali,” amesema Dk. Tumaini.
Alieleza kuwa kwa sasa chuo hicho kina wanafunzi 3,000 wa kozi ndefu na 5,000 hadi 6,000 ambao ni wa kozi fupi za kila mwaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Kepteni Ernest Bupamba, amesema wamepata maeneo Mwanza na Lindi kwa ajili ya kujenga matawi ya DMI.
“Kule Mwanza tutajenga tawi letu ili kufundisha vijana jinsi ya kuunda meli na kule Lindi tutajenga kwa ajili ya kuwafundisha kutengeneza majahazi,” amesema,” Bupamba.
Amesema baharini kuna rasilimali kama gesi na mafuta na pia Kuna utalii ambao ni muhimu kwa chuo hicho kuandaa wataalam ambao wataongoza watu kuutembelea baharini.
Aidha amesema Chuo hicho kina kazi ya kutangaza fursa zilizomo baharini ikiwa ni pamoja na kufanya makongamano kama haya yanayokutanisha wadau mbalimbali.