Christina Gauluhanga -Dar es Salaam
WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa ya kusoma vyuo vya elimu ya juu nje ya nchi ili kupata ujuzi unaoendana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia.
Wito huo umetolewa mwishoni wiki na mwambata mwenza wa Taasisi ya Elimu ya Juu ya Edugate ya nchini Uingereza, Aliyuthuman Sadhique wakati wa uzinduzi wa programu maalumu ya kusaidia wanafunzi katika nchi zenye uchumi wa kati inayofahamika kama LICAP.
Sadhique alisema programu hiyo inalenga kuwafikia wanafunzi na wahitimu mbalimbali kutimiza malengo katika vyuo maalumu vilivyopo Uingereza na Sri Lanka.
“Edugate kwa kushirikiana na Taasisi ya British College of Applies Studies ya Sri Lanka, tumedhamiria kuwekeza katika elimu hapa nchini, hususan kuwawezesha Watanzania kwenda kusoma nje ya nchi, ikiwamo kuwasaidia kimasomo,” alisema Sadhique.
Alisema wamezindua programu hiyo ambayo itaaendana na kongamano maalumu litakalotoa fursa kwa Watanzania kuzitambua fursa hizo za elimu.
Aliwataka wale wote wenye nia ya kusoma nje ya nchi kuhudhuria kongamano hilo na kwamba litakuwa na faida kubwa hususan kwa wahitimu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (IT), usimamizi wa fedha, uhandisi na taaluma zingine.
Alisema kwa wale ambao ufaulu wao utaonekana kuwa ni wa juu, watasaidiwa kupata udhamini kupitia programu hiyo ya LICAP. Mmoja wa waratibu wa kongamano hilo, David Munanka, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka ambao Serikali ya awamu ya tano inatekeleza dira yake ya kuelekea uchumi wa viwanda.