27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Watahadharishwa kuhusu mikopo kausha damu

Na Mwandishi wetu, Kigoma

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, Kanali Isack Mwakisu amewataka wananchi kukopa kwenye taasisi za fedha zilizosajiliwa na kutambulika kwa kuwa itasaidia kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwa mkopaji kwa kuwa taasisi hizo zinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria.

Kanalı Mwakisu alitoa rai hiyo baada ya kukutana na wataalam wa Wizara ya Fedha, TAMISEMI, Benki Kuu na wataalam wengine kutoka Taasisi za Serikali waliofika wilayani mwake kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali.

Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa wananchi wanatakiwa kwenda kukopa fedha kwenye benki na taasisi nyingine za fedha zilizosajiliwa na zinazotambulika kisheria na siyo kwenda kukopa kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa na serikali.

“Matumizi ya fedha ni muhimu sana, hivyo wananchi wasikope tu kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa”. amesisitiza Kanali Mwakisu.

Aidha, Kanali Mwakisu amesema Serikali imekusudia kuhakikisha wananchi wengi wanapata uelewa wa masuala ya fedha ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika huduma rasmi za fedha.

“Wakulima msifanye matumizi mabaya ya fedha zenu mnapo vuna mazao yenu bali fedha hizo zitumieni kwenye matumizi sahihi ikiwemo kupeleka watoto shule,” amesema .

Kwa upande wake Stanley Kibakaya ambaye ni Ofisa Usimamizi wa Fedha, Wizara ya Fedha, amewataka wananchi wanapokopa waangalie viwango vya riba ndipo wakope na kuhakikisha wanabaki na nakala ya mkataba ili panapotokea changamoto mkataba huo uwalinde.

Kwa upande wake, Abonaventula Frederick, mkaazi wa Kasulu aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kutoa elimu hiyo ambapo aliiomba Serikali kuendelea kutoa maeneo mengine kwani asilimia kubwa ya wananchi hawajui wapi wanatakiwa kuhifadhi fedha zao na wapi wanatakiwa wakope.

“Wananchi wengi hawajui wapi pakuhifadhi fedha zao na wengi wamekopa sehemu ambazo siyo sahihi hali ambayo imesababisha wauze mali zao ikiwemo mashamba ili walipe mikopo wanayodaiwa, hivyo wengi wakipata elimu hii wataelimika,”amesema Frederick.

Naye Stephanie Fulmasi amesema kuwa wamepata elimu kupitia filamu ambayo imeandaliwa na Wizara hiyo na kupitia filamu hiyo wamejifunza namna gani wakina mama wanatakiwa kwenda kukopa sehemu sahihi na siyo kukopa sehemu yenye riba kubwa.”

Mafunzo ya elimu ya fedha yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Fedha yanalengo la kufikisha elimu na uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha.Kata zilizofikiwa mpaka sasa ni Buhingwe, Mnanila, Kinazi, Kasulu, Makere – VETA na Mvugwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles