MORONI, COMORO
MAHAKAMA Kuu Comoro imewatangaza wagombea 13 watakaoshiriki Uchaguzi wa Rais mwezi ujao ikiwazuia wapinzani wakuu wa Rais Azali Assoumani.
Wagombea 19 walijiandikisha kwa ajili ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Machi 24 na kati ya waliopitishwa, ni Rais Azali pekee anayewakilisha chama cha siasa.
Wengine wote wanashiriki kama wagombea binafsi katika uchaguzi huo, ambao unatarajia kumrudisha madarakani Azali aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2016.
Wapinzani wake wakuu walikuwa Makamu Rais wa zamani, Mohamed Ali Soilih na Ibrahim Mohamed Soule, ambao juhudi zao za kuwania wadhifa huo zilitupiliwa mbali na mahakama iliyojaa washirika wa Azali.
Mpango wa kupokezana madaraka miongoni mwa visiwa vitatu vya taifa hilo ulisaidia kuzuia hali ya kutoridhika iliyotawala kwa miaka kadhaa pamoja na mapinduzi ya mara kwa mara mwishoni mwa miaka ya 1990.
Uchaguzi utafanyika kwa mujibu wa vifungu vya Katiba vilivyorekebishwa kwa utashi wa Rais Azali katika kura ya maoni iliyofanyika Julai 2018.
Mageuzi hayo yanamwezesha rais kushika madaraka kwa mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja badala ya muhula mmoja.
Iwapo Azali atashinda, atachukuliwa kuwa ndiyo anaanza muhula wake wa kwanza, jambo ambalo litamruhusu kuwania muhula wa pili mwaka 2024.
Soilihi alisema amezuiwa kugombea kwa tuhuma kuwa alificha umiliki wa kampuni yenye thamani ya mabilioni ambayo amekana kuifahamu.
“Wagombea wote wa upinzani ambao wangetoa changamoto kwa Azali wamezuiwa,” alisema, na kupinga kile alichokiita ucheleweshaji wa uchaguzi.
Soule alisema alizuiwa kwa sababu hati yake ilisainiwa na Naibu Katibu Mkuu badala ya Katibu Mkuu, Ahmed el-Barwane, ambaye alikuwa gerezani kwa miezi kadhaa kwa madai ya kumshambulia mwanajeshi.
Upinzani umeparaganyika baada ya viongozi wake kadhaa kukamatwa.
Mahakama ya Usalama imetoa hukumu kadhaa za vifungo jela kwa wanasiasa mashuhuri waliopinga kura ya maoni inayomruhusu Azali kurefusha muhula wake madarakani.
Ikiwa awamu ya pili itahitajika kwa kukosa mshindi wa moja kwa moja, itafanyika Aprili 21.
Katiba mpya imebakisha mzunguko wa urais miongoni mwa visiwa vitatu vya Grande Comore, Anjouane na Moheli, lakini kipindi kimeongezwa kutoka miaka mitano hadi 10.
Kisiwa cha Azali cha Grande Comore, hivi sasa ndiyo kinashikilia fursa hiyo.
Azali mwenyewe alianza kutwaa madaraka kwa njia ya mapinduzi dhidi ya kaimu rais mwaka 1999 na alirudishwa madarakani hadi 2006 katika uchaguzi wa vyama vingi.
Hii leo wakosoaji wa Azali wanachukulia kwamba amechukua mwelekeo wa udikteta, akiwa na uwezekano wa kubaki madarakani hadi 2029.