NAIROBI, KENYA
WAFUASI wa Muungano wa Upinzani Kenya, National Super Alliance (NASA), wameandamana katika baadhi ya miji nchini humo kutaka kuondolewa kazini kwa baadhi ya maofisa wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Maofisa wa Usalama Kenya, wamekuwa wakifanya doria karibu na jumba la Anniversary Towers zilipo ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), jijini Nairobi.
Muungano wa Nasa ukiongozwa na Raila Odinga, umetangaza maandamano ya kila Jumatatu na Ijumaa kushinikiza kuondolewa kwa Ofisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Ezra Chiloba na maofisa wengine wakuu kwa tuhuma za kuhusika katika makosa yaliyochangia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8, mwaka huu.
Uchaguzi mpya wan chi hiyo umepangwa kufanyika Oktoba 26, mwaka huu, lakini NASA wanataka mabadiliko yafanywe kwenye tume hiyo kabla ya kukubali kushiriki katika uchaguzi huo.
Katika uchaguzi uliofutwa, IEBC ilimtangaza Uhuru Kenyatta wa Chama cha Jubilee kuwa mshindi wa nafasi ya urais kwa kupata kura 8, 203, 290 ambayo ni asilimia 54.27 , huku mpinzani wake mkuu, mgombea wa muungano wa NASA, Raila Odinga akipata kura 6,762,224 ambayo ni asilimia 44.74.