Na Nyemo Malecela, Kagera
Kufuatia kuripotiwa kwa matukio mengi ya mauaji na migogoro mbalimba mkoani Kagera, viongozi wa dini mkoani humo wameshauriwa kuacha tabia ya kushabikia mambo yanayoipinga serikali ili kuondoa hali ya kutokuamiwa na kushirikishwa katika mambo yanayohitaji msaada wa viongozi hao.
Hayo yamesemwa na Askofu wa Kanisa la Calvary Assemblies of God jimbo la Kagera (CAG), Damian Rwabitikula katika kongamano la viongozi wa dini wa jimbo hilo lililofanyika Kata ya Chonyonyo wilayani Karagwe mkoani humo.
Askofu Rwabitikula alisema kutokana na matukio ya mauaji yanayoripotiwa ndani ya Mkoa huu mara kwa mara, viongiozi hao wanatakiwa kutoweka ushabiki na uchochezi bali waisaidie serikali katika kuwahubili waumini ili waondokane na hali ya vitendo hivyo.
“Wachungaji ni watu wa kuaminiwa tangu enzi, ni kioo cha jamii na ili uaminiwe na kuheshimiwa na unaowaongoza inatakiwa kutengeneza imani kwa serikali ili taifa linapohitaji majibu liyapate kutoka kwao,” alisema.
Alisema kwa Mkoa wa Kagera ambao umepakana na nchi zaidi ya tatu umekuwa na matukio mengi ya unyang’anyi, mauaji, migogoro ya ardhi jambo linaloleta taharuki kwa wananchi na kupelekea serikali kutafutia ufumbuzi kwa kushirikisha kamati za amani za Mkoa zinazosimamiwa na viongozi wa dini zote.
Alisema bado serikali ina imani na viongozi wa dini kupitia maandiko ya Biblia katika kuwahubilia na kuwaaminisha watu kuacha maovu ambayo yanafanywa kwenye jamii ambayo huondoa amani kwa hofu ya maisha.
Alisema bado serikali ina imani na viongozi wa dini kupitia maandiko ya Biblia katika kuwahubilia na kuwaaminisha watu kuacha maovu ambayo yanafanywa kwenye jamii ambayo huondoa amani kwa hofu ya maisha.
Katibu Msaidizi wa Kanisa la The Love of Calvary Church kutoka Arusha, Mwalimu Lodrick Daffa alisema miongozo ya dini inayohusu viongozi hao ni maono, mpangilio wa kazi, nidhamu, mawasiliano na uhusiano katika utendaji wa kazi zao.
Aidha alisema endapo viongozi wakiwemo wachungaji watafuata mambo hayo itawasaidia kufanana na nafasi zao wanazoziongoza pamoja na kuwa msaada kwa kusaidia kuweka msisitizo kwenye jamii juu ya mambo yanayosisitizwa na wataalamu wa Serikali kwa wananchi.
Katibu wa kanisa hilo Mkoa wa Kagera, Mchungaji Agnes Charles amesisitiza wachungaji wawe na utamaduni wa kujiendeleza kielimu kwa kushiriki mafunzo mbalimbali ya uongozi ili kujikumbusha miiko na maadili katika kazi yao.
“Mnatakiwa kujiongezea upeo kwa kushiriki mafunzo mbalimbali ya uongozi yatakayowasaidia kuongeza nguvu katika maombi, kujielewa, kuelewa nani aliyewaita katika huduma, msiangalie upinzani unaowakabili katika kazi zenu na badala yake kuongeza jitihada na ubunifu katika kazi ili kuweza kuendana na wakati ulipo sasa,” alisema Charles.