30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

WAONGOZAJI MAKINI WATASAIDIA KURUDISHA BONGO MUVI

Na RAMADHANI MASENGA

UMEIONA tamthilia ya Siri ya Mtungi? Umeitazama mara ngapi? Umemwangalia Duma wa Siri ya Mtungi? Umemtazama Duma wa filamu zingine? Achana na huyo.

Njoo kwa Wema Sepetu na Rose Ndauka. Umewatazama mara ngapi katika muvi walizocheza na marehemu Kanumba, marehemu Adam Kuambiana ama na JB? Umewatazama mara ngapi wakiwa katika filamu nyingine na wasanii wengine?

Wote hao niliotaja ni wasanii wenye vipaji vikubwa. Ila ubora na ukali wao huwa unapungua katika baadhi ya filamu na kuzidi katika filamu nyingine. Kwa mfano kina Wema wakiwa na Kanumba wanakuwa wasanii hatari kwelikweli.

Kila muda ukiwaangalia unafurahi kuwatazama, kila wanachofanya katika muvi unakiona kama hakiigizwi. Ni raha sana kuona muvi za Wema au Rose Ndauka akiwa chini ya JB au kipindi kile akiwa akiongozwa na Adam Kuambiana au  Kanumba.

Ukimtazama Duma katika Siri ya Mtungi utachanganyikiwa. Utajiuliza maswali mengi kwanini umechelewa kumjua. Utashangaa kwanini baadhi ya wasanii ni mashuhuri kuliko yeye? Kwanini kwenye filamu nyingine hatishi?

Tanzania tuko makini sana kutafuta waigizaji huku tukisahau kutafuta waongozaji makini. Filamu ikiwa na mwongozaji makini hata kama kuna wasanii wa kawaida wataonekana bora.

Ukiangalia sinema za kina Kanumba, Ray au za JB na nyingine zilizoongozwa na Adam Kuambiana utaelewa nini namaanisha.

Patcho Mwamba akiwa anaigiza na wasanii wengine unaweza usishtuke sana. Ila mtazame Patcho katika filamu akiwa na JB, Kanumba au Kuambiana utapagawa. Unamuona anatisha zaidi.

Lafudhi yake ya Kikongo, mapigo yake ya mavazi na mapozi yake yatakufanya utamani kumuona kila mara. Ila huyohuyo akiwa katika filamu na wengine unashangaa. Anapwaya, anaonekana anafanya kitu ambacho hakiwezi vizuri.

Tanzania bado tuna shida kubwa sana ya waongozaji filamu. Nimejaribu kuangalia filamu nyingi kutoka Chuo cha Sanaa Bagamoyo, zinafurahisha, zinaburudisha na wala huoni kama kuna maigizo ndani yake.

Unakumbuka ile Tamthilia ya Rama na Zawadi kutoka Bagamoyo? Unakumbuka weledi, umakini wa waigizaji na utamu wa stori ile? Hivi ndivyo vitu tunavyokosa sasa katika filamu zetu.

Tanzania tuna wasanii wengi wazuri ila bahati mbaya waongozaji ni wachache sana. Wengi wanajiita waongozaji ila ni vituko tu.

Hata tamthilia za Kaole Sanaa Group zilitukosha kwa sababu ya kuwa na waongozaji wazuri na makini. Hata filamu za  Tuesday Kihangala huwa zinaburudisha kutokana na uongozi wake.

Wakati tukiwa katika uelekeo wa kuinua soko la filamu Tanzania, basi suala la waongozaji makini nalo lipewe kipaumbele. Unaweza kuandaa mazingira mazuri ya soko, Serikali inaweza kuwekeza nguvu za kutosha kama sasa inavyoonekana ila kama hakuna waongozaji wazuri basi hatutopata filamu zenye ubora na hivyo kupelekea soko kupata anguko jingine kubwa kama ilivyotokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles