Baadhi ya wanawake wanaokwepa kunyonyesha watoto kwa hofu ya kupoteza mvuto wako hatarini kupata saratani ya matiti kulinganisha na wanaonyonyesha.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Crispin Kahesa amewashauri wanawake kuhakikisha wananyonyesha watoto kulingana na jinsi inavyoshauriwa na wataalamu wa lishe.
Amesema miaka ya karibuni imeibuka tabia kwa baadhi ya wanawake kukwepa jukumu hilo na kuongeza kuwa matiti kwa mwanamke pamoja na kwamba hutengeneza maziwa ambayo ni chakula cha mtoto pia ni sehemu ya mwili ambayo wengi huitumia kama urembo kwa ajili ya kuongeza mvuto.
“Kila mwaka tunapokea wagonjwa wapya wapatao 5,500 ambapo kati yao 700 huwa wana saratani ya matiti ambao ni sawa na asilimia 12 ya wagonjwa wote tunaowapokea, wengi huja ugonjwa ukiwa katika hatua ya tatu na nne ambazo ni hatari zaidi na huwa ni vigumu kupona.
“Kibailojia mwanamke ana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti kuliko mwanaume kwani ana kiwango kikubwa cha homoni ya Oestrojeni,” amesema.