NA BENJAMIN MASESE,
SIKU moja baada ya polisi kunasa silaha nzito za vita, mabomu yaa kurusha kwa mkono ndani ya nyumba moja iliyopa Bukaga Kata Kishili, wananchi wa eneo hilo wamevamia makazi hayo na kugawana vitu vyote vilivyokuwamo na kuichoma moto.
Mwishoni mwa wiki, polisi wakiongozwa na Kamanda wa Mkoa huo, Ahmed Msangi, walivamia nyumba hiyo na kuwakamata watu 17 wakiwamo watoto 11 wanaodaiwa kufundishwa mafunzo ya gaidi.
Vilevile ilikamatwa bundi ya AK 47, mabomu ya kurusha kwa mkono, visu, majambia, magazine tano zilizokuwa na risasi 150 na bunduki aina ya Mark 4 na vitu vingine.
Kutokana na hali hiyo, wananchi walivamia nyumba hiyo na kujichukulia kila kilichokuwamo na baadaye kuichoma moto huku wakidai kuwa mali hizo zimepatikana kwa damu za binadamu.
Pia wananchi hao walisisitiza kwamba kamwe hawatakubali kuona familia au ndugu wakijaribu kufika eneo hilo kwa kutaka kuendeleza makazi hayo.
Waliwaomba viongozi wao kuanzia mtaa hadi kata kuanza hatua za kuchukua kiwanja hicho kwa ajili ya kujenga ofisi ya umma na hata kituo cha polisi.
Wakati wote tukio hilo hakuna kiongozi wa mtaa wala kata aliyekuwapo na kila mmoja hakutaka kutaja jina lake.
MTANZANIA ilishuhudia jinsi wananchi walivyokuwa wakivunja nyumba hiyo ambako wanaume walijikita katika kutoa mabati, milango na mageti ya chuma huku kinamama wakihaha kuchukua vitu vya ndani.
“Yaani kama unatafuta mali kwa damu ya watu, mwisho wa siku ndiyo kama haya yanakukuta, sasa kwa kuwa hizi mali zilizotokana na damu za wenzetu basi zinarudi kwa wenyewe, hatutaki familia hii au ukoo uje hapa.
“Tunaomba eneo hili lichukuliwe na Serikali kwa matumizi ya umma, hatutakuwa tayari kuona tunaishi na magaidi, tunaliomba jeshi la polisi lisiwaachie hao watu, wakija hapa tutawamaliza ,”alisikika kijana mmoja.