Na Ashura Kazinja – Kilosa
WANANCHI wa Kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wameiomba Serikali kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo migogoro ya ardhi, ukosefu wa maji safi na salama pamoja na miundombinu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, mgombea udiwani Kata ya Dumila aliyepitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Deogratias Mwigunila wakati wa utambulisho wa mgombea ubunge wa jimbo hilo na madiwani.
Alisema mbali na mafanikio mengi yaliyopatikana kipindi cha miaka mitano, ikiwamo uboreshaji wa utoaji elimu ya msingi na sekondari, hospitali na vifaa tiba, lakini bado kuna changamoto zinazotakiwa kufuatilia.
Akizitaja changamoto hizo, alisema ni upatikanaji wa maji safi na salama, miundombinu, maji na umeme Kijiji cha Mkundi, aliiomba Serikali kuwatatulia changamoto hizo.
“Mamilioni ya shilingi yameshatolewa kwenye mradi wa maji kwa ajili ya kupeleka maji vijiji vitatu, hautoi maji vizuri, wanaonufaika ni wa Dumila tu, nimeomba hata kabla ya uchaguzi maji yaanze kutoka,” alisema.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mbunge mteule wa Jimbo la Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi aliwashukuru wananchi kwa kumdhamini na imani kubwa waliyoionyesha kumkubali kugombea ubunge.
Aliwahakikishia kuwatumikia vema sambamba na kuwa kiongozi anayefikika, na kuwaomba kushirikiana kwa pamoja katika kutatua matatizo na changamoto zinazowakabili.
“Nimekuja kuwashukuru wananchi na wana CCM wa Kilosa kwa imani kubwa mliyonipa na kunithamini, nisingekuwa na sifa ya kugombea kama msingenikubali.
“Niwahakikishie nimekuja kuwatumikia, nitajitahidi kuwa mbunge ninayefikika, ndugu ni kwa mama, nimerudi nyumbani, nimekulia huku,” alisema Kabudi.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kilosa, Raphael Mwita alisema jimbo hilo lina kata 40, kati ya hizo 22 wagombea wamepita bila kupingwa na uchaguzi utakuwa kwenye kata tisa tu.