Na JOSEPH LINO
WANAFUNZI wengi hawajui nini cha kuandika katika wasifu (CV) mara baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu. Wengi hawajui waandike nini au vitu ambavyo havipaswi kuwapo kwenye CV.
Kuandika CV kwa mara yako ya kwanza ni mchakato ambao unaweza kukuondolea kujiamini.
Utafiti uliofanywa na taasisi ya ajira za mtandao ya The Ladders, umebainisha kuwa waajiri wengi hutumia wastani wa sekunde sita kuangalia CV kabla hawajaamua kuchukua mtu sahihi.
Mtaalamu wa Taalum wa The Ladders, Amanda Augustine anasema hakuna sheria ngumu ya kuandika CV, inategemea kile ambacho unapaswa kukiandika kama unaweza kukifanyia kazi. Kuna miongozo ya awali ya wanafunzi au wataalamu waliomaliza masomo na hawana uzoefu.
“Kuwapo katika soko la ajira baada ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu ni jambo la furaha na la kusisimua. Lakini wahitimu wengi hujikuta wakikabiliwa na changamoto ya kuhitaji uzoefu wa kupata kazi, unahitaji kazi ili kupata uzoefu,” anasema.
Kwa bahati nzuri, ujuzi ambao waajiri huthamini zaidi haupatikani tu katika ulimwengu wa ajira bali mbinu za kuandika wasifu bila ya kuwa na uzoefu wa kazi. Namna unavyoiandika kwa umahiri unaweza kuonesha ujuzi utakaomhamasisha mwaajiri kukuona wewe ni bora.
Namna ya kuandika CV bila kutaja uzoefu wa kazi:
Tambua sifa zako muhimu
Kuandika CV kimsingi ni namna ya kujiweka katika hali ya kujiuza kikazi. Kitu cha kwanza ni kujua au kuwa na kielelezo cha kitu unachokiuza, tengeneza orodha ya vitu vyote unavyoweza kufanya bila kujali kama una sifa za kitaaluma au hapana. Kisha, linganisha orodha ya sifa za waajiri wanaotafuta.
Anza na maelezo binafsi
Hiki ni kitu cha kwanza kabisa ambacho mwajiri yeyote huwa anaanza kukisoma. Hivyo, andika kwa makini. Maelezo yanahitaji kuwa mafupi iwezekanavyo wastani wa maneno 150.
Anza kwa kujitambulisha kwa kiwango chako cha elimu na ujuzi wako mfano; “Mimi hufanya kazi kwa juhudi kubwa na mwenye kujitegemea ambaye nimehitimu hivi majuzi.
Kisha ongezea kwa kuweka shahada uliyosomea au chuo kikuu kama unahisi ni muhimu kulingana na jukumu la kazi unayoomba.
Hakikisha unataja moja kwa moja kazi unayoombwa au taja kazi unayotafuta lakini pia weka chaguo lako wazi kwa ujumla.
Taja ujuzi wako badala ya majukumu
CV nyingi huanza kwa kuweka orodha ya ajira ambazo umewahi kufanya, lakini kama hujafanya kazi kabla au umefanya kazi katika sekta isiyo rasmi, ni vyema zaidi kuanza na ujuzi ulionao. Hakika waajiri wataiona kuwa ni ya kuvutia na muhimu zaidi.
Usisahau ujuzi wa kawaida
Je! una leseni ya dereva? Je, unaweza kutumia programu mbalimbali za kompyuta? Je, una uelewa wa mitandao ya kijamii? Mara nyingi, wahitimu wengi huacha ujuzi ambao waajiri wanataka kwa sababu wanafikiri kuwa si muhimu.
Ikiwa unaweza kufanya kitu ambacho kinaweza kuwa na manufaa katika sehemu ya kazi, hasa utumiaji wa programu za kompyuta, lugha ambazo unaweza kuzungumza. Uzoefu wa kuzungumza lugha fulani ni muhimu, pia usidanganye uwezo wako kwa kila jambo.