NA JOSEPH LINO
KUNA baadhi ya watu huwa wanazaliwa na akili za ajabu na wenye vipaji vya hali ya juu.
Tumekuwa tukisikia uwezo wa watoto ambao hufanya vizuri darasani hadi kusababisha kuhitimu elimu ya chuo kikuu wakiwa wadogo kwa sababu ya kurukishwa madarasa.
Kwa kipindi kirefu wamekuwapo au wapo watu ambao walivunja historia ya kutunikiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) wakiwa na umri mdogo kutokana na kuwa na akili za kipekee (genius) na hivyo kufunya maajabu katika ulimwengu wa elimu.
Wiki hii tunaangalia wanafunzi wenye umri mdogo waliofanikiwa kupata PhD wakiwa kati ya umri wa miaka 13 hadi 20.
Wanafunzi wengine walionyesha maajabu, baada ya kuzaliwa waliweza kuongea lugha mbalimbali, kusoma au kufanya hisabati hata kabla hawajaanza shule ya awali.
Hawa ni baadhi ya watu waliovunja rekodi kwa kupata shahada ya uzamivu wakiwa na umri mdogo.
Karl Witte (13)
Karl Witte, raia wa Ujerumani alizaliwa mwaka 1800 baba yake alikuwa akimhimiza kusoma na kujihusisha na masuala mbalimbali kitoto. Witte akiwa na miaka tisa aliweza kuzungumza lugha kadhaa ikiwamo Kijerumani, Kifaransa, Kitaliano, Kilatini na Kigiriki.
Alipokuwa mtoto alihudhuria Chuo Kikuu cha Giessen nchini Ujerumani na alihitimu na kupata PhD akiwa na miaka 13. Bado hadi sasa hakuna aliyevunja rekodi yake.
Baba ambaye alikuwa mchungaji aliandika kitabu kinachoitwa The Education of Karl Witte au The Training of a Child.
Kitabu hicho kilipingwa na kukosolewa nchini humo na hakikufanikiwa. Hata hivyo, kitabu hicho kilifanya vizuri nchini China na kuvunja rekodi ya mauzo hadi kufikia mwanzoni mwa karne ya 21.
Mamilioni ya raia wa China waliamini kwamba mtoto wao angeweza kuwa kama Witte kwa kusomo kitabu hicho.
Maisha ya Witte yalikuwa siri na magumu kuthamini na inasemekana alisafiri kwenda Italia mwaka 1818 na alitaka kuwa mwanasheria.
 Kim Ung-Yong ( 15)
Kim Yong alizaliwa mwaka 1962, nchini Korea Kusini na ametajwa kuwa mtu mwenye kiwango kikubwa cha akili (intelligence quotient IQ) cha 210.
Alianza kuzungumza akiwa na umri wa miezi sita na alielewa kufafanua Hisabati hasa zile za algebra akiwa na miezi minane.
Alipofikisha miaka miwili aliweza kuzungumza Kijapani, Kikorea, Kijerumani na Kiingereza kwa ufasaha.
Mwaka 1967 alionekana kwenye kipindi cha moja kwa moja katika kituo cha luninga cha Fuju TV nchini Japani akifumbua hesabu za algebra.
Yong akiwa na miaka mitatu hadi sita alikuwa anahudhuria masomo ya Fikizia katika chuo kikuu cha Hanyang Korea Kusini, alipofikisha miaka saba, Shirika la Anga la Marekani (NASA) lilimkaribisha kwenda nchini humo na kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Colorado akiwa mwanafunzi wa PhD, ambapo alitunikiwa akiwa na miaka 15.
Mwaka 1974, aliajiriwa na NASA akiwa mtafiti ambapo alifanya kazi kwa miaka minne. Hata hivyo, alihisi kubanwa na huku kazi zote alizokuwa akifanya zilikuwa zinaenda kwenye shirika hilo, hivyo mwaka 1978 akaamua kurudi Korea Kusini ambapo alifanikiwa kupata PhD ya pili katika taaluma ya uhandisi. Hadi sasa Yong ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Chungbuk nchini humo.