26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi NIT watengeneza mifumo kudhibiti uvuvi haramu, wizi wa magari

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wametengeneza mifumo itakayosaidia kukomesha wizi wa magari na uvuvi haramu.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jangwani wakipata maelezo kutoka kwa Sumai Reuben wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambaye ametengeneza mfumo wa kufuatilia matumizi ya gesi nyumbani.

Mifumo hiyo ambayo baadhi yake imeanza kutumiwa na chuo hicho imekuwa kivutio katika Maonyesho ya Sita ya Wahandisi Wanawake Tanzania (TAWECE) yanayofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wakizungumza katika maonyesho hayo walimu wa wanafunzi hao, Doreen Sarwatt na Pricila Ishabakaki wamesema hatua hiyo ni sehemu ya mafunzo kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi pindi wanapohitimu waweze kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii.

Kuhusu mfumo wa kudhibiti uvuvi haramu, Sarwatt amesema unawasaidia wavuvi wasivue katika maeneo yasiyoruhusiwa ambapo mvuvi hutaarifiwa kupitia simu ya mkononi iwapo atavua eneo lisiloruhusiwa.

Amesema mfumo mwingine ni wa mizigo ambapo kama unasafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine muhusika atajua uzito wake na iwapo umeshafika eneo unakokusudiwa.

“Hizi ni baadhi ya ‘project’ nzuri ndiyo maana tumezileta kwenye maonyesho na wanafunzi unaowaona ndiyo waliozitengeneza,” amesema Sarwat.

Naye Pricila Ishabakaki ambaye ni Mhandisi upande wa Mawasiliano Pepe, amesema wanafunzi wake wametengeneza mfumo wa kusaidia mafundi katika karakana za magari na wa kufuatilia matumizi ya gesi nyumbani.

“Mara nyingi tunatumia gesi na hujui lini itaisha, kwahiyo wametengeneza mfumo ambao unafuatilia kiwango cha gesi kila wakati na inapokaribia kuisha inamfahamisha mtumiaji kupitia ujumbe mfupi wa simu na ‘alarm’. Ikitokea gesi inavuja mfumo utatoa taarifa kwa mtumiaji,” amesema Ishabakaki.

Getrude Magesa anayesoma uhandisi wa magari katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) akionyesha mfumo alioutengeneza wa kusaidia mafundi katika karakara za magari.

Amesema mfumo mwingine umetengenezwa na wanafunzi wanaosoma uhandisi wa magari ambao unamwezesha mtumiaji wa gari kuliwasha kwa kutumia ‘bluetooth’ au alama ya kidole badala ya funguo na kusaidia kupunguza wizi wa magari.

Aidha amesema kupitia kitengo cha ujasiriamali cha chuo hicho miradi yote inayoonekana ina faida kwa jamii hurasimishwa na kwamba mingine tayari wameanza kuitumia katika karakana ya chuo hicho.

Naye Sumai Reuben ambaye ametengeneza mfumo wa kufuatilia matumizi ya gesi nyumbani amesema ataendelea kutumia vema taaluma aliyoipata ili kutatua changamoto zilizoko kwenye jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles