Na Allani Vicent, Tabora
Wanachama na mashabiki wa Klabu ya Simba inayoshiriki ligi kuu soka Tanzania Bara Tawi la Sikonge mkoani Tabora wamejipanga kujenga kituo cha uwekezaji kitakachotumika kama kitega uchumi cha tawi hilo.
Wakizungumza na Mtazania Digital walisema kuwa eneo la ujenzi wa  Kituo hicho tayari limeshapatikana na sasa wanaendelea kukusanya michango kutoka kwa wanachama wenzao ili kufanikisha mradi huo.
Mwenyekiti wa Tawi hilo, Charles Wamlyoma alisema kituo hicho kitakuwa na eneo la ofisi, ukumbi, vyumba zaidi ya 18 vya maduka ya biashara ambavyo vitapangishwa kwa wafanyabiashara na eneo la kupumzikia.
Alibainisha kuwa jengo hilo litakuwa mali ya wanachama wa klabu hiyo tawi la Sikonge na mapato yote yatakayopatikana yataingizwa katika akaunti ya chama na wanachama ndiyo watakaoamua nini cha kufanya na fedha hizo.
Naye Katibu wa Tawi hilo Hamis Kimwaga alisema kuwa hadi sasa wameshakusanya zaidi ya Sh 310,000 kwa ajili ya mradi huo na juhudi zaidi zinaendelea kufanywa ili kupata michango zaidi.
Mweka hazina wa tawi hilo, Celina Mbadagu alisema kituo hicho ni muhimu sana kwa kuwa kitafungua fursa mpya za kibiashara kwa wakazi wa wilaya hiyo na maeneo jirani ikiwemo kuendeleza vipaji vya soka.
Aidha, aliongeza katika kituo hicho watauza vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo jezi za Simba, viatu, mipira na vifaa vinginevyo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Peresi Magiri aliwapongeza kwa maono mazuri na kuahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma yao ya kujenga kituo hicho ambacho kitasaidia kutoa ajira kwa vijana wenzao.
Kwa upande wake shabiki wa klabu hiyo na Mjumbe wa Kamati Tendaji, Mfaume Zahoro alimshukuru Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara kwa kukubali mwaliko wao wa kuja kuzindua tawi jipya la timu hiyo, kutembelea eneo la ujenzi wa kitega uchumi na kuahidi kuwasaidia.