Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Benki ya NMB imepokelewa kwa mikono miwili visiwani Zanzibar katika kuhakikisha inapeleka mbele mikakati ya kufikia uchumi wa Blue hasa kwa upande wa kukuza utalii.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Juni 20, 2021 na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah alipomwakilisha Rais wa visiwa hvyo, Dk. Hussein Mwenye kwenye hafla ya uzinduzi wa umoja wa wamiliki wa hoteli Zanzibar, (Hotel Association Zanzibar – HAZ).
Amesema kitendo walichokionyesha Benki ya NMB kuwa mdhamini mkuu wa hafla ya uzinduzi wa HAZ kinadhihirisha dhamira ya dhati waliyokuwa nayo katika kukuza utalii visiwani Zanzibar, bila kujali hali ya sasa ya kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.
“Tunaipokea Benki ya NMB kwa mikono miwili visiwani Zanzibar, uwekezaji wa hoteli unazidi kukua na hamkukosea kulenga sekta hii ya hoteli. Idadi ya hoteli inakua kwa kasi Zanzibar ambapo mwaka 2018 zilikuwepo hoteli 509 na sasa zimefikia 620, yaani kwa mwaka zinaongezeka hoteli kati ya 25 hadi 36,” amesema Abdallah.
Alibainisha, ili serikali itimize malengo yake inategemea kwa kiasi kikubwa wawekezaji, ndiyo maana wameamua kufungua milango ili wawekezaji wa ndani na nje wapate fursa za kukuza biashara na kuanzia biashara mpya.
“Taasisi hii niliyoizindua leo (HAZ) ina wanachama takriban 30, lakini hoteli zipo nyingi na kwa takwimu inaonyesha wamiliki wa hoteli ndio walipaji wazuri wa kodi Zanzibar, hivyo tunaamini kuanzishwa kwa taasisi hii ni hatua kubwa ya kuitangaza Zanzibar kimataifa kuwa ni kituo muhimu kwa utalii,” amesema Abdallah.
Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi amesema biashara ya hoteli inachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Zanzibar, hivyo anaamini fursa ni kubwa hasa ikizingatiwa zaidi ya hoteli 500 zilizopo ikiwa ni sawa na zaidi ya vitanda 900, Zanzibar inaweza kupokea wageni wengi ikiwa kutakuwa na ubunifu wa kutosha.
“Benki ya NMB imekuwa ikifanya vizuri katika biashara kwa miaka zaidi ya 10 mfulululizo, ni benki pekee inayotengeneza faida kubwa lakini pia imefika maeneo mengi Tanzania, kama hiyo haitoshi ndiyo benki pekee inayoweza kutoa mkopo mkubwa kwa mteja mmoja kwa wakati mmoja, Benki ya NMB inaweza kutoa mkopo wa zaidi ya Sh bilioni 200 kwa mteja mmoja bila kutikisika,” amesema Mponzi na kubainisha:
“Tumesikia pia kilio chenu wamiliki wa hoteli juu majanga ya moto na changamoto ya kutopata fidia kwa wakati, Benki ya NMB tunawahakikishia kuwa utaratibu wetu wa bima ni wa kipekee na unamhakikishia mteja kupata fidia yake yote kwa wakati,”.
Katika hatua nyingine, Mponzi alisema Benki ya NMB imefungua fursa pana kwa Zanzibar, kwa sasa kuna ATM 17 ambapo zipo nyingine saba zinaongezwa kaika maeneo mbalimbali ikiwemo ATM inayotoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni itakayowekwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume uliomalizika kujengwa hivi karibuni.
Aidha, benki hiyo inahudumia zaidi ya wateja 60,000 visiwani humo ambapo vilevile ipo huduma ya wateja binafsi, huduma ambayo inampa fursa mteja kupata wasaa wa kufanya miamala kwa utulivu na upekee.
Vilevile, katika kuhakikisha wageni hawapati tabu katika kupata huduma ya malazi na kutembelea maeneo ya kitalii, Beki ya NMB inaweza kutoa fursa ya mteja kufanya malipo akiwa popote duniani kwa kutumia mfumo wa malipo ya kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa HAZ, Paolo Rosso alisema wana imani kubwa Benki ya NMB itawapa mwanzo mpya kutokana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo hasa ikizingatiwa taasisi hiyo ni changa.