Na JUDITH NYANGE-MWANZA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limetumia mabomu ya machozi kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga waliokuwa wakifanya biashara zao mbele ya Msikiti wa Madhehebu ya Kihindu na Shule ya Awali ya Rajendra iliyopo eneo la Makoroboi.
Polisi walilazimika kutumia nguvu baada ya wafanyabiashara hao kuanza kuwarushia mawe mgambo wa jiji waliofika kuwaondoa katika eneo hilo kuanzia saa 12 alfajiri ili wasipange bidhaa zao kutokana kukwamisha shughuli za ibada kwa waumini wa misikiti hiyo kiasi cha kufunga barabara na lango la kuingia ndani.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema walilazimika kutumia nguvu ya ziada baada ya wamachinga hao kutumia mawe kuwashambulia mgambo wa jiji waliokuwa wakiowaondoa na baada ya kutaarifiwa ndipo polisi walipofika na kudhibiti hali hiyo.
“Katika eneo hilo la Makoroboi waumini wa msikiti walilalamika kushindwa kuendelea na taratibu zao kutokana na machinga kulitumia vibaya tamko la rais kwa kufunga barabara pamoja na lango kuu la msikiti na hivyo kuzuia shughuli za kijamii pamoja na swala kuendelea ndani ya msikiti kutokana na kelele.
“Walifikisha malalamiko yao kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ambaye leo ilibidi kuwaondoa katika eneo hilo kutokana na kushindwa kufuata utaratibu, lakini mgambo wa jiji walianza kurushiwa mawe na tulilazimika kuingilia kuwatuliza machinga hao na hadi sasa tunawashikilia watu wanane waliokuwa wakirusha mawe ambao tutawafikisha mahakamani,” alisema Msangi.
Aliwataka wafanyabiashara hao kutotumia vibaya matamko ya Rais Dk. John Magufuli na badala yake wafanye shughuli zao kwa mujibu wa utaratibu hadi pale utaratibu wa kuwapeleka katika maeneo waliyotengewa utakapokamilika.
Akizungumza na gazeti hili jana mmoja wa wafanyabiashara hao, Said Juma, alisema alifika katika eneo hilo mapema jana na kukuta askari na mgambo wa jiji wametanda katika eneo hilo na aliwakataza kuingia na kuendelea kufanya biashara katika eneo hilo.
Alisema baada ya muda kidogo kupita walikuwa wamefika na walijaribu kuwaomba askari hao kuingia na kuchukua mizigo pamoja na meza zao lakini walikataa kuwaruhusu.
Mfanyabiashara mwingine ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alisema alishangaa kwanini wanaondolewa katika eneo hilo wakati Rais Magufuli alitoa agizo wasiondolewe katika maeneo hayo hadi pale watakapotafutiwa maeneo mengine.
“Nashangaa kwanini tunaondolewa katika eneo letu la biashara bila kuelekezwa tuende wapi ambapo tutaendelea kufanya biashara zetu kama ilivyokuwa katika eneo hilo, mwishoni mwa wiki iliyopita waumini wa huu msikiti walituomba tuwapishe kuanzia Ijumaa hadi Jumanne ili waweze kusherehekea sherehe zao tulikubali na kuwapisha hapa biashara tumeanza kupanga Jumatano,” alisema.
Naye Godfrey John, alisema huenda polisi wamelazimika kuwaondoa wafanyabiashara hao katika eneo hilo baada ya kukithiri kwa vitendo visivyo vya kibinadamu walivyokuwa wakivifanya.
“Unajua hawa wamachinga walikuwa wakipanga bidhaa zao hadi mbele ya geti la kuingia msikitini, hata mtu akitaka kuingia au kutoka na gari anashindwa, lakini waumini wa msikiti huo waliwavumilia.
“Kama hiyo haitoshi walikuwa wakijisaidia haja ndogo katika chupa tupu za maji na kuzirusha ndani ya eneo la msikiti pamoja na kuharibu kuta za msikiti kwa kugonga misumari ili watundike bidhaa zao, hata kama ingekuwa wewe mwandishi lazima ungekereka na tabia hiyo,” alisema John.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema yupo kikaoni.