27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Waliozidi uzito wapewa rufaa kwenda Muhimbili

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Asilimia 82 ya wananchi waliopimwa uzito katika banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili kwenye maonyesho yanayoendelea ya Sabasaba wamegundulika kuwa na uzito uliozidi na kupewa rufaa ya kwenda hospitali kwa uchunguzi zaidi.

Mmoja wa wananchi akipimwa uzito katika banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili kwenye maonyesho ya Sabasaba yanayoendelea.

Akizungumza na Mtanzania Digital, Ofisa Lishe Mwandamizi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Scholastica Mlinda, amesema wanachofanya katika maonyesho hayo ni kujenga uelewa lakini wengi wamewashauri kufika hospitali ili kuwachunguza kwa kina.

“Wengi waliokuja hapa (Sabasaba) tumewapa rufaa waje kufanya vipimo zaidi kwa sababu kuongezeka uzito si suala la kula peke yake. Mtu anakula nini, analala muda gani, anafanya nini, anatumia dawa labda za muda mrefu kwahiyo inahitajika uchunguzi zaidi ili hata unapomshauri awe anajua anafanya nini na kwa sababu gani.

“Kuna vipimo vingine vya kuwafanyia ili kujua kwenye uzito alionao je, ni mafuta kiasi gani ametunza mwilini, protin ni kiasi gani, mifupa yake imetunza madini kiasi gani na majimaji na damu mwilini vina uzito kiasi gani.

“Mfano anayenyanyua vyuma anaweza akawa na kilo 100 lakini hizo si za mafuta ni za misuli na kuna mwingine anaweza akawa na kilo 100 lakini nusu ya kilo alizonazo ni mafuta, na ndiyo hao wenye vitambi,” amesema Mlinda.

Amesema wamebaini bado watu wana ulaji mbovu hawafuati misingi ya afya hasa ulaji sahihi wa vyakula ndiyo maana wengi wana uzito uliokithiri.

“Wengi wanakula vyakula vya wanga, mafuta na sukari na kutokula kiasi kingi cha mbogamboga na matunda hasa yasiyokuwa na sukari, vyakula hivi huchangia kwenye ongezeko la uzito.

“Uzito uliozidi unaambatana na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, moyo, saratani, figo kwahiyo hii si afya sana hasa kwa watu tuliowaona ambao wengi wako katika umri wa uzalishaji.

“Kama watu wengi tuliowaona wenye uzito mkubwa na uliopitiliza wako kwenye viashiria vya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza, huko mbeleni gharama za matibabu kwa serikali zitakuwa kubwa. Kwa sababu magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanachukua muda mrefu,” amesema.

Amesema lishe ni mfumo wa maisha hivyo wameelimisha umma juu ya ulaji sahihi kulingana na kazi mtu anazofanya na umri wake na kuhamasisha ulaji wa mbogamboga na matunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles