Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WABUNGE wa CCM wanaodaiwa kuhusika na mikataba ya madini inayolalamikiwa, wamechangia fedha wakati wa harambee ya ujenzi wa jengo la kisasa la makao makuu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), linalotarajia kujengwa Dodoma.
Wabunge hao, Andrew Chenge wa Bariadi, Dk. Dalaly Kafumu wa Igunga na William Ngeleja wa Sengerema, walichanga fedha hizo jana.
Harambee hiyo iliongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai. Pia, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda alikuwapo.
Wakati wa harambee hiyo, Dk. Kafumu na Chenge waliahidi kuchanga Sh 500,000 kila mmoja na Ngeleja aliahidi kuchanga Sh milioni 3 kupitia kwa mwakilishi wake ambaye pia ni Mbunge wa Ulanga, Gudluck Mlinga (CCM).
Kabla ya harambee hiyo ilifanyika sala maalum ya kuliwekea wakfu jengo hilo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk. Alex Malasusa.
Baada ya sala hiyo kumalizika, Spika Ndugai alipewa kipaza sauti kwa kuongoza harambee ambako aliwataja Chenge na Dk. Kafumu kuwa waliahidi kuchangia kila mmoja Sh 500,000 huku yeye mwenyewe akiahidi kuchanga Sh milioni 10 kwa ajili ya ujenzi huo.
Mbali na kina Chenge, Spika aliwataja wabunge wengine wa CCM walioahidi kuchangia ujenzi huo na fedha zao kwenye mabano kuwa ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (Sh 500,000), Mbunge wa Makambako, Deo Sanga (Sh 500,000), Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko (Sh 200,000) na Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje aliyeahidi kuchangia Sh 300,000.
Wakati Mlinga akizungumzia ahadi itakayotolewa na Ngeleja, alisema walikubaliana kiasi atakachotoa yeye (Mlinga), Ngeleja atoa mara mbili ya kiasi hicho.
‘’Mimi nachangia shilingi milioni moja na nusu, lakini Mheshimiwa Ngeleja aliniagiza kiasi nitakachochangia mimi, yeye atachangia mara mbili yangu. Kwa hiyo, yeye atatoa shilingi milioni tatu kwa sababu mimi nitatoa shilingi milioni moja na nusu,” alisema Mlinga.
Wabunge wengine waliochangia harambee hiyo ni Mbunge wa Kilolo,Venance Mwamoto na wabunge wa Viti Maalum CCM, Felister Bura, Josephine Ngezabuke na Dk. Christine Ishengoma.
Wakati hao wakitoa ahadi hizo, Pinda aliahidi kutoa Sh milioni nne, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde aliahidi kutoa Sh milioni mbili na Mbunge wa Newala, George Mkuchika aliahidi kutoa Sh 500,000.
Katika mazungumzo yake wakati wa harambee hiyo, Spika Ndugai alisema lazima Watanzania wanufaike na rasilimali zilizopo nchini yakiwamo madini.
“Tunashukuru kwa maombi haya mnamuombea rais wetu, Dk. John Magufuli, maana shetani anasimama hapa na pale hasa katika nyakati hizi ambazo tunapita katika mazingira ambayo sasa Watanzania tunaamka.
“Watanzania sasa lazima tuanze kuona rasilimali zetu zinatunufaisha ingawa miongoni mwetu kuna watu wanataka, wanadhani ni vema tukaendelea na hali hii.
“Ili kitu kiitwe raslimali ni lazima kiwe na thamani ,kama hakina thamani huwezi kukiita raslimali. Yaani kama unapita njiani na kukuta shanga moja imedondoka njiani, huwezi kupoteza muda wako kuiokota, lakini ukikuta almasi ya saizi hiyo hiyo, utachekelea kwa sababu utajua umepata raslimali.
“Kwa hiyo, kama hatupati faida kupitia madini yetu, misitu yetu na samaki wetu, hatuwezi kuviita raslimali kwa sababu hatunufaiki navyo,” alisema Spika Ndugai.
Naye Dk. Malasusa alisema CCT iliziunga mkono jitihada za Hayati Mwalimu Nyerere kwa kuamua kuhamia Dodoma tangu mwaka 1986 baada ya kutangazwa mwaka 1973.
Pinda aliwataka Watanzania kuwa na moyo wa kushukuru kwa kuwa kila jambo linawezekana mbele za Mungu.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CCT, Canon Matonya, alisema jengo hilo litakuwa la kisasa na litagharimu Sh bilioni tatu.
Katika harambee hiyo, zaidi ya Sh milioni 147 zilipatikana huku ahadi zikiwa ni Sh milioni 87.47.