Na Renatha Kipaka, Bukoba
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali​ Charles Mbuge amewataka wakuu wa Wilaya kuwa wabunifu kwenye maeneo yao ili kupata miradi mingi zaidi na kuacha kutegemea iliyopo siku zote.
Mbuge ameyasema hayo leo Jumanne Juni 22, 2021 wakati akiapisha wakuu wa wilaya​ tatu zilizopata viongozi wapya katika nafasi hiyo na kusema kwamba​ kiongozi anapoingia katika nafasi lazima aache alama kama ukumbusho hata kwa vizazi vinavyofuata.
“Unapoaminiwa na kupewa nafasi unapaswa kuwa mbunifu na mwadilifu ili kuzitumia fursa zilizopo kwenye wilaya uliyokabidhiwa,”amesema Mbunge.
Amesema kufanya hivyo nikuondoa umaskini katika mkoa kwa kuunda miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kuongeza kipato kwa wananchi.
Amefafanua zaidi kuwa mkoa una raslimali za kilimo, uvuvi na ufungaji, hivyo ni jukumu la kuangalia wapi sehemu ya kukaa na kuboresha na kuanzisha utendaji kazi.
Aidha, amesema kuna miradi mingi ambayo haikukamiliki kwa wakati tatizo likiwa ni usimamizi uliopo chini ya kiwango na usioridhisha.
Awali, akizungumza kwa niaba ya wakuu wawilaya, Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Moses Machali alisema, ushirikiano wa wananchi ndiyo wenye kuongeza chachu ya maendeleo.
Machali amesema majukumu ya kiongozi ni kupata dhamila ya kuleta maendeleo na kutenda kazi ya kuongeza uchumi
Katibu Tawala wa mkoa Kagera, Profesa Faustine Kamzora amesema fursa nyingi zinapatikana mkoani hapo ambazo zikitumiwa na viongozi zinaweza kwenda mikoa ya nchi jirani.
“Kutoka hapa mkoani kwenda mikoa iliyopo nchi jirani nikaribu sana kwenda mikoa inayopatikana ndani ya mikoa yetu ni suala tu la kuangalia usalama ambao hautaleta uvunjifu wa amani,” amesema Kamzora.
Amesema utendaji kazi na usimamizi wa majukumu ndiyo njia ya kupata kipato ambacho kitainua maendeleo ya mkoa.
Hata hivyo wakuu wa wilaya walioapa kwa ajili la kuanza majukumu ni mkuu wa wilaya ya Karagwe, Julieth​ Binyula, wilaya ya Misenyi Kanali Wilson Sakulo, wilaya ya Biharamulo Kemilembe Lwota.