Na RAMADHAN LIBENANGA– MOROGOROÂ
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu wawili kwa   kupatikana na kilo moja ya dawa za kulevya (cocaine) na pembe za ndovu mbili zenye thamani ya Sh milioni 33.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,Urlich Matei alisema Juni 30   usiku, askari wakiwa kwenye doria ya kawaida maeneo ya Msamvu Manispaa ya Morogoro, walimkamata Sunday Balinos mkazi wa Msamvu akiwa na dawa za kulevya  katika mfuko wa rambo uliozungushiwa gundi ya plastiki.
Alisema   mtuhumiwa yupo rumande anaendelea kuhojiwa I kujua mtandao wa dawa hizo   na baadaye atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Kamanda Matei alisema pia kuwa Juni 29 mwaka huu   asubuhi   katika   Tarafa ya Mlali wilayani Mvomero, askari wakiwa kwenye doria walimkamata Kimosa Kibona (43) mkazi wa Mlali akiwa na pembe mbili za meno ya tembo zenye thamani ya Sh milioni 33.
Alisema  polisi walipokea taarifa za intelijensia na kuweza kumkamata mtu huyo akiwa ameziweka nyara hizo za Serikali kwenye mfuko wa rambo.
Katika tukio la tatu, Jeshi la Polisi linamshikilia  Stephan  Felician (32) mkazi wa Mbezi  Dar es Salaam kwa   kukutwa na debe moja la bangi.
“Mtuhumiwa alikamatwa akiwa kwenye Kituo cha Mabasi  Msamvu,” alisema Kamanda Matei.