Na Allan Vicent, Tabora
Wakulima wa tumbaku mkoani Tabora wanatarajia kuuza zaidi ya kilo milioni 14 katika msimu huu wa masoko baada ya vyama vya msingi 91 wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika (WETCU 2018 LTD) kuingia mkataba na makapuni 5 ambayo yamewaongezea makisio ya kuzalisha kilo 14,460,000.
Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Chama hicho aliyemaliza muda wake, Mrisho Simba alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji shughuli za Chama katika kikao cha mkutano mkuu wa mwaka.
Alisema katika mkataba huo makisio ya kilo zitakazozalishwa na kununuliwa kwa kila wilaya sasa itakuwa Sikonge kilo 6,657,000, Tabora Manispaa kilo 742,000, Nzega kilo 372,000 na Uyui kilo 6,689,000.
Alibainisha kuwa katika msimu wa 2020/21 Chama Kikuu cha Ushirika kilichukua hatua mbalimbali zilizolenga kuboresha kilimo cha zao hilo ikiwemo kuhamasisha matumizi sahihi ya pembejeo na kutafuta masoko zaidi.
Mrisho aliongeza kuwa wamekuwa wakihamasisha vyama vya msingi wakiwemo wakulima binafsi kulima mazao mbadala ikiwemo alizeti, ufuta, korosho na pamba huku akibainisha kuwa baadhi wameanza kunufaika na mazao hayo.
“Mpango tulio nao sasa ni kuendelea kuhamasisha kilimo cha mazao mbadala hususani korosho ili nalo liingizwe rasmi na kusimamiwa na vyama vya ushirika vya msingi ili kurahisisha utafutaji masoko,” alisema.
Mrisho alisisitiza kuwa makampuni yote yanahitaji tumbaku bora ambayo inaweza kushindana kwenye soko la Kimataifa, hivyo ni wajibu wa kila mkulima kuzalisha tumbaku bora ili makampuni hayo yaendelee kuwepo na mengine yaje.
“Katika msimu wa 2020/2021 vyama wanachama 91vilipata mikopo ya benki kati ya vyama wanachama 129, vyama 38 havikushiriki kilimo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo madeni, kutopata mgao na kutokuwa na maandalizi,” alisema Mrisho.
Meneja wa WETCU, Samwel Jokeya alisema katika kuhakikisha tumbaku yote inayozalishwa na wakulima wa vyama vya msingi mkoani humo inanunuliwa, makampuni mapya 3 yamesaini mikataba ya kuzalisha kilo 4,530,000 katika msimu huu hivyo kuongeza makisio ya tumbaku itakayonunuliwa, alitaja makampuni hayo kuwa ni PACHTEC, NAILE na ENVY SERVICES LTD.
Aliongeza kuwa Chama Kikuu nacho kwa kutambua kuwa kina jukumu la kutafuta masoko kimesaini mikataba ya uzalishaji wa kilo 470,000 na vyama 4 wanachama hivyo kuongeza matumaini makubwa ya kununuliwa tumbaku yote.