Na JANETH MUSHI -ARUSHA
WAKILI Median Mwale na wenzake watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka 44, jana waliibua taharuki mahakamani baada ya kuachiwa huru na kutimua mbio kabla ya kukamatwa na polisi.
Wakili Mwale na wenzake, Don Bosco Gichana raia wa Kenya, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi, waliachiwa huru baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kukubaliana na ombi la Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), la kuondoa shauri la mahakamani.
Baada ya kuachiwa huru, Wakili Mwale na mwenzake walibaini kuwepo kwa polisi waliokuwa wakisubili kuwakamata tena, hivyo waliamua kuwakwepa kwa kutimua mbio tukio ambalo lilizua taharuki katika viunga vya mahakama.
Akisoma uamuzi wa kuwaachia huru Wakili Mwale na wenzake katika kesi ya Jinai namba 61 ya mwaka 2015, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, David Mrango alikubaliana na ombi la DPP lililowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali na kumtaka asiwakamate tena.
Hata hivyo, baada ya Wakili Mwale na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka 44 yakiwamo ya utakatishaji fedha, kughushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu, polisi na askari kanzu waliokuwa mahakamani walianza kuwafuata.
Wakili Mwale na wenzake waliokuwa wameambatana na familia zao na mawakili wanaowatetea baada ya kubaini wanafuatwa walitimua mbio huku polisi wakiwafuata.
Polisi walimkamata kwanza Ndejembi aliyekuwa akishuka ngazi na mkewe ambaye alianza kupiga picha tukio hilo kwa simu yake ya mkononi kabla naye ya kutiwa nguvuni.
Mwale na wenzake wawili walijaribu kuwakimbia polisi kwa kuruka uzio wa jengo la Don Bosco lakini walikamatwa kabla hawajatokomea.
Tukio hilo la askari kanzu, polisi na watuhumiwa kufukuza, lilivuta hisia za mawakili, mahakimu na watu waliokuwa mahakamani hapo na wakati likiendelea polisi waliwaondoa washtakiwa eneo hilo kwa kutumia magari ya polisi yaliyokuwa na namba za usajili T 770 CWT, T 953 CZS aina ya TDI na PT 3766.
Wakili Mwale na wenzake walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mwaka 2011.
NDANI YA MAHAKAMA
Awali, mahakama iliwaachia huru washtakiwa huku ikikubaliana na ombi lililowasilishwa juzi na  mawakili wa utetezi kuwa wasikamatwe tena kwa vile maombi ya DPP yamelenga kuwatesa wateja wao na siyo  mara ya kwanza kwa kesi hiyo kuomba iondolewe.
Jaji Mrango alisema mahakama haina mamlaka ya kukataa maombi ya DDP lakini alisisitiza kuwa endapo wameyawasilisha kwa nia njema shauri hilo liondolewa na washtakiwa wasikamatwe.
Wakili wa utetezi, Albert Msando juzi akiwasilisha pingamizi hilo aliieleza Mahakama kuwa DPP alitakiwa kutoa sababu za kutokuendelea na kesi kwa sababu alikuwa na muda wa miaka miwili kufanya hivyo.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyekomya akisaidiana na mawakili waandamizi, Shadrack Kimaro na Pius Hilla na upande wa utetezi uliongozwa na Wakili Albert Msando akisaidiwa na mawakili Omary Omary, Mosses Mahuna, Innocent Mwanga na Buheri Ngoseki.
Akiwasilisha ombi la DPP mahakamani, Wakili Tibabyekomya alieleza kuwa DPP anaomba chini ya Kifungu cha 91(1) cha mwenendo wa makosa ya jinai kuondoa shauri hilo na kwamba ombi hilo liingizwe kwenye kumbukumbu za mahakama.
Hii ni mara ya pili kwa DPP kuondoa shauri hilo mahakamani, mara ya kwanza ilikuwa Novemba 23, mwaka 2015, ambapo liliondolewa kisha washitakiwa hao walikamatwa na kufunguliwa kesi upya.