PATRICIA KIMELEMETA NA MANENO SELANYIKA
WAKILI wa mmiliki wa IPTL, Harbinder Seth, Joseph Sungwa, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mteja wake apelekwe Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji wa maradhi ya puto yanayomkabili.
Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara, James Rugemarila, ambao wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwamo ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Kimarekani 22,198,544.60 na Sh 309,46,300,150.27.
Wakili Sungwa alitoa ombi hilo jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Alidai mteja wake Seth anatakiwa kwenda Afrika Kusini kuonana na daktari wake ili afanyiwe upasuaji wa ‘puto’ lililopo tumboni.
“Mheshimiwa bado Seth anasumbuliwa na madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na mpaka sasa hawajaweza kumfanyia upasuaji hivyo ni vyema mahakama ikatoa amri ili akatibiwe na daktari wake aliyeko Afrika Kusini,” alidai Sungwa.
Alidai kuwa Muhimbili bado haina uwezo na teknolojia ya kufanya upasuaji na kutoa hilo puto, hivyo basi ni vema mahakama hiyo ikatoa kibali ili aweze kutibiwa kwa madai kuwa muda wake unakaribia kuisha.
Wakili Sungwa aliuomba upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi haraka kwa sababu ni miezi mitano sasa upelelezi haujakamilika kwani si haki ukizingatia umri na tatizo la kiafya walilonalo washtakiwa.
Akijibu kuhusu matibabu ya Seth, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai kuwa bado hawajapokea ripoti maalumu kutoka kwa daktari ya kuthibitisha kuwa puto la Seth limemalizika muda wake.
Alidai haoni sababu ya kusafirishwa hadi Afrika Kusini kwa kuwa Tanzania wapo madaktari wa kutibu ugonjwa wake.
“Kuhusu suala la upelelezi umefikia hatua nzuri kwa sababu tumeiomba mahakama itupe ruhusa kwenda kuchukua maelezo kwa washtakiwa hivyo tunaomba muda,” alidai Swai.
Aliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, Hakimu Shaidi, aliwataka upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi unakamilika ili washtakiwa wapate haki yao na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 24, mwaka huu.