Veronica Romwald na Julieth Julius-
Dar es Salaam
WATU 15 wanaoishi katika Bonde la Msimbazi, wamekamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wakidaiwa kukaidi amri ya kuhama katika maeneo hayo.
Askari wa Jeshi hilo walifanikiwa kuwakamata watu hao kwa kushirikiana na viongozi wa Manispaa ya Ilala, walipofanya operesheni kali ya kuwakamata watu wanaoendelea kuishi kwenye maeneo hatarishi ya mabondeni eneo la Buguruni, Kata ya Vingunguti.
Kamishna wa Kanda hiyo, Simon Sirro, aliwaeleza hayo waandishi wa habari jana ofisini kwake kwamba, operesheni hiyo ilifanyika Machi 15, mwaka huu katika maeneo hayo.
“Operesheni hii inafanyika kufuatia kukiukwa kwa amri ya mahakama inayowataka watu hao kuhama katika maeneo hayo hatarishi kufuatia kuwepo kwa mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko,” alisema.
Aliwataja waliokamatwa ni Mohamed Hatibu, Mwanaidi Mwinyimvua, Kulwa Antony, Mwanahamisi Ally, Sophia Mwinjuma, Salim Juma, Mwajuma Athumani, Saada Said, Sabahi Abdallah, Mariam Abbasi, Ashura Petro, Fitina Mohamed, Faudhia Juma, Magreth John, Ayoub Abdallah.
“Watu hawa wanatoka katika familia tofauti tofauti, tumewahoji na wamekiri kuendelea kukaa katika maeneo hayo hatarishi na kwamba wanasubiri maelekezo kutoka kwa Serikali,” alisema Kamishna Sirro na kuongeza:
“Watuhumiwa hao wameachiwa kwa dhamana na kwamba upelelezi bado unaendelea na pindi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.”
Wakati huo huo, Kamishna Sirro alisisitiza wananchi kuendelea kushiriki katika ulinzi shirikishi kwenye maeneo yao kwani suala hilo lipo kwa mujibu wa Katiba.
“Jiji la Dar es Salaam limekua, sasa hivi kuna watu zaidi ya milioni sita, tupo askari zaidi ya 6,000, kwa idadi hii inamaanisha kila askari anapaswa kulinda raia zaidi ya 1,000 wao na mali zao jambo ambalo ni changamoto.
“Awali tulilazimika kuzuia ulinzi shirikishi kwa sababu watu walianzisha tu wenyewe na badala ya kulinda maeneo yao walikuwa wanakwenda kulinda mitaa mingine, huu ni ubabaishaji ambao ulisababisha vitendo vya rushwa na uhalifu na wananchi wakaanza kulalamika.
“Lakini vikundi vinavyoanzishwa sasa, vinasimamiwa na Mwenyekiti wa Mtaa husika ambao kwa mujibu wa sheria ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika mtaa husika,” alisema.
Kamishna Sirro alisema kwa kuwa vikundi hivyo vipo chini ya wenyeviti, ulinzi shirikishi sasa umeanza kuzaa matunda.
“Kwa mfano katika Wilaya ya Temeke kulikuwa na matukio mengi ya uhalifu lakini leo yamepungua kwa sababu ya ulinzi shirikishi, kwa hiyo ni wakati wa vikundi vilivyopo kujitathmini kama wanaweza kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria za nchi na wawe na maadili na kazi wanayofanya,” alisema.
Alisema jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua wale watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwani hawatachukuliwa kama wana vikundi wa ulinzi shirikishi bali wahalifu kama wahalifu wengine.