Na Beatrice Kaiza, Mtanzania Digital
Zaidi ya wajasiriamali 195 kutoka Mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani wamejitokeza katika banda la SIDO wakijumuisha wajasiriamali wa programu maalumu ya ubunifu na kuongeza tija kwenye uzalishaji.
Mwitikio huo wa wajasiriamali na wananchi kutembelea banda la SIDO umeonyesha mafanikio ya huduma zinazotolewa na SIDO na uhitaji wa huduma hizo kwa wale ambao hawajafanikiwa.
Hayo yameelezwa Julai 7, 2023 na Mkurugenzi Mkuu SIDO, Mhandisi Sylvester Mpanduji wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Banda lao la SIDO wakati wa Maonyesho ya 47 ya Kimataifa ya biashara (Sabasaba) yenye kaulimbiu ya ‘Tanzania ni Mahali sahihi pa Uwekezaji na Biashara’.
“Maonyesho haya ni fursa ya kipekee ya kuonyesha na kutambulisha bidhaa na mashine zinazozalishwa na viwanda vidogo na vya kati hapa nchini ikiwemo vituo vya SIDO vya Teknolojia vinavyozalisha mashine na vipuri mbalimbali,” amesema Mhandisi Mpanduji.
Aidha, Mhandisi Mpanduji amezitaja aina mbalimbali za Teknolojia zenye kuongeza thamani ya mazao mbalimbali ambazo zinapatikana ndani ya Banda lao la SIDO.
“Ndani ya banda la SIDO kipekee mtaweza kuona aina mbalimbali za mashine za mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu, madini zikiwemo za mashine za kusindika mazao ya mahindi, matunda, asali, alizeti, mpunga, karanga, Mchikichi, muhogo, korosho.
“Pia zitakuwepo mashine za utengenezaji wa bidhaa za ngozi, usindikaji wa maziwa, utengenezaji sabuni, mishumaa, chaki, ujenzi, upuraji wa nafaka, mashine za vyakula vya mifugo, ukataji nyasi,” amesema Mhandisi Mpanduji.
Ameongeza kuwa bidhaa nyingine ni za usindikaji vyakula kama vile viungo vya chakula, uyoga, samli, mafuta ya alizeti, mboga za majani zilizokaushwa na asali kutoka Tabora.
Mbali na hayo amewakaribisha wananchi wote kwenye maonesho ya nne ya kitaifa yatakayofanyika mkoani Njombe kuanzia Oktoba 21 hadi 31, mwaka huu yenye kaulimbiu ya ‘Pamoja tujenge viwanda kwa uchumi na ajira endelevu’
“Maonesho haya ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kutathimini, kupenda na kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vidogo na vya kati nchini ili kuongeza tija ya uzalishaji katika viwanda na ajira endelevu,” amesema.