Na Clara Matimo, Mwanza
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, amewataka waumuni wa dini ya kiislamu mkoani humo, kujiepusha na migogoro baina yao na viongozi wa dini na serikali ili kuendelea kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano ambayo ndiyo mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Sheikh Kabeke ametoa rai hiyo leo Mei 3, jijini hapa wakati akiswalisha swala ya Eid el fitri iliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Nyamagana na kuwakutanisha mamia ya waumini wa dini ya kiislamu kutoka maeneo mbalimbali mkoani humo .
“hata ikitokea jambo kubwa namna gani mmesikia kuna mtafaruku labda wa masheikh wanarumbana huyu anasema vile nyie waumini msiingilie kati nyie tazamani kaeni kimya na niwaase masheikh mbalimbali katika mambo ambayo tunatofautiana wasituwekee misimamo ya kutugawa waisilamu, isiwe sababu ya sisi waisilamu kufarakana,”amesema na kuongeza.
“Na waumini wa dini ya kiisilamu tusikubali viongozi watugawe wala wananchi wachache wasiopenda amani tusikubali wakatugombanisha na viongozi wetu, serikali ina nia njema na raia wake hivyo tuwape ushirikiano ili waweze kututatulia changamoto mbalimbali zinazotukabili kitaifa,” amesema Sheikh Kabeke.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi, ambaye alihudhuria swala hiyto amewataka waumin wa dini hiyo kuwa makini na watoto wao katika siku hizi za sikukuu endapo wataenda nao maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutembea.
“ Wale ambao mtakuwa mmetoka na watoto wenu kwenda kwenye maeneo mbalimbali kufurahi kwa ajili ya sikukuu hakikisheni mnakuwa makini katika kuwaangalia watoto ili wasipate madhira yoyote na jeshi la polisi tuko kazini muda wote nawaomba tupeni ushirikiano,”amesema Nganzi.
Baadhi ya waumini wa dini hiyo akiwemo Ashura Mohamed, amewataka waislamu wenzake kuendelea kutenda matendo mema “Tuendeleza yale yote ambayo tumeyafanya katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kusaidiana, kuoneana huruma, kuwasaidia wahitaji , kuwasalimia waginjwa na mengine mema ambayo Mwenyezi Mungu ametuagiza tuyatende, kwa kufanya hivyo tutapata kuiona pepo,”amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, amesema,“Kama mtu alikuwa ameacha yale madhambi ambayo anatambua kabisa hayampendezi Mwenyezi Mungu ikiwemo pombe aache moja kwa moja, twende na kamba ya Mwenyezi Mungu tuwe na tabia njema lakini tuwe na upendo mkubwa tushirikiane na kuhakikisha tunasimama na kamba ya Mwenyezi Mungu,”.