FRANCIS GODWIN, IRINGA
WAHITIMU wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa mkoani Iringa, wameipongeza Serikali kwa kuwadhamini masomo yao kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
Akitoa pongezi kwa niaba ya wenzake kupitia hotuba ya wahitimu hao, Philemon Frugence ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Elimu katika Sayansi mwaka 2018/19, alisema pasipo udhamini wa mikopo ya Serikali, ingekuwa ni vigumu kwa wengi wao kumaliza masomo yao.
Akisoma hotuba hiyo mbele ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete juzi wakati wa mahafali ya 11 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa Iringa, Frugence alisema wengi wa wanafunzi waliohitimu ni watoto wanaotoka familia duni kiuchumi, hivyo udhamini huo umewapatia haki watoto wote kupata elimu ya juu.
Alisema pamoja na Serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, bado zipo changamoto mbalimbali ambazo wanaomba iendelee kuzitatua katika chuo hicho.
“Mkuu wa chuo safari yetu hapa chuoni haikuwa fupi na tambarare kama wengi walivyodhani, bali ilikuwa ni ndefu yenye milima na mabonde.
“Miongoni mwa sababu zilizosababisha safari yetu kuwa ndefu ni pamoja na upungufu wa vyumba vya hosteli. Changamoto ya malazi kwa wanafunzi itarudia kila mwaka katika hotuba za wanafunzi kutokana na umuhimu wake mkubwa,” alisema Frugence.
Alisema kukosekana kwa malazi ndani ya chuo kumewafanya wengi wao kuendelea kuishi nje ya chuo na maisha ya nje ya chuo yamegubikwa na hofu ya kiusalama, hasa wakati wa usiku wanapotakiwa kwenda kujisomea ndani ya chuo.
“Tumekuwa tukihofu kuvamiwa na kuibiwa mali zetu, kelele za watu tunaoishi nao mitaani ni nyingi, kama walevi na muziki ambao ni vigumu kuuzuia kutokana na kuwa maeneo yasiyo rafiki ya kujisomea kwa utulivu huko mitaani, kwani wanaishi maeneo ya biashara za wananchi,” alisema Frugence.
Alisema changamoto nyingine ni bei kubwa ya pango na unyanyasaji unaofanywa na wamiliki wa nyumba walizopanga wanafunzi mitaani nje ya chuo.
Frugence alisema Serikali ili kusaidia wanafunzi kuondokana na changamoto hizo, ni vema kujenga hosteli za kutosha ndani ya chuo ili waweze kuishi katika mazingira salama kielimu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa chuo hicho na Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Wiliam Anangisye alisema bodi ya usimamizi inachukulia mahafali hayo kama matokeo ya jukumu lake la msingi la usimamizi wa chuo hicho.
Alisema bodi imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia shughuli zote za chuo, ambazo ni kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali ya chuo kwa miaka mitano (2016/17 -2019/20) na sera mbalimbali zinazotungwa.
Kuhusu changamoto ya ukosefu wa malazi, alisema imeendelea kuwa kero kwa wanafunzi.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jaji mstaafu Damian Lubuva aliipongeza Serikali kwa kudhamini idadi kubwa ya wahitimu kupitia HESLB.