Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
HOMA ya pambano la watani wa jadi Simba na Yanga, imezidi kupanda baada ya kuwaibua wachezaji wa zamani wa timu hizo kutoa mitazamo yao kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kupigwa kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni miongoni mwa mechi za watani zenye hamasa kubwa barani Afrika, ukishika nafasi ya tano kutokana na kubeba hisia za mashabiki wa soka nchini, huku pande zote mbili zikijinadi kushinda pambano hilo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, beki wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, Boniface Pawasa, alisema matokeo ya mchezo huo yataamuliwa na timu itakayoweza kutumia vyema nafasi itakazopata kwenye mechi hiyo.
Alisema kikosi chao kinabidi kuwa makini na Ibrahimu Ajib kwani ndiye mchezaji tishio zaidi na atainyima Simba ushindi endapo atapewa nafasi ya kuuchezea mpira.
“Simba iko vizuri kuliko Yanga, kwani kila mtu anaweza kufunga tofauti na wenzetu ambao wanamtegemea zaidi Ajib kuwapa matokeo, kwenye kikosi hata ukimzuia Emmanuel Okwi, bado timu inaweza kuvuna pointi tatu kupitia kwa Laudit Mavugo na John Bocco.
Beki huyo alisema kiungo Mohamed Ibrahim ‘Mo’, hatajwi kuelekea mchezo huo, lakini akipewa nafasi na kocha Joseph Omog ataipa Simba ushindi na kuwalaza Yanga mapema.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba, alisema wachezaji wa Yanga wamkabe Okwi kwani ndiye anayewapa jeuri ya kutamba Wekundu hao wa Msimbazi.
“Simba ina jicho moja tu kwenye mchezo huo, ukifanikiwa kumbana Okwi, basi umewamaliza, tunalijua hilo hivyo hawatupi shida.
“Wao wana mfungaji mmoja pekee, kwetu hata wakimkaba Ajib, Amissi Tambwe na Donald Ngoma, wanaweza kufunga, hivyo tuamini tutaibuka na ushindi kwenye mchezo huo kutokana na uzoefu walionao wachezaji wetu, alisema Mziba ambaye wakati akicheza alifahamika zaidi kwa jina la Tekelo.
Timu hizo zinaendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo huo, ambapo Simba inatarajia kurudi kesho asubuh ikitokea Zanzibar wakati Yanga inawasili leo ikitokea Morogoro.
Mchezo huo utakuwa wa nne kwa timu hizo kukutana kwa mwaka huu, kwani tayari zimekutana katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi na mchezo wa Ngao ya Jamii.
Yanga ikiwa chini ya Mzambia George Lwandamina, haijafanikiwa kuibuka na ushindi katika mpambano huo baada ya kupoteza michezo hiyo mitatu, huku akiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Agosti 23 mwaka huu na Simba kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3.