Mwandishi Wetu
TAASISI ya Wanawake Wahasibu nchini ( TAWCA) imesema moja ya malengo yao makuu ni kuhakikisha wanaanzisha benki yao siku za karibuni na wanaamini hakuna kitakachowakwamisha katika kufanikisha lengo hilo.
Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa Pili wa TAWCA uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAWCA Neema Kiure-Mssusa amewaeleza washiriki zaidi ya 300 waliohudhuria mkutano huo kuwa lengo la kuanzishwa kwa benki litafanikiwa na mikakati waliyoiweka inakwenda vizuri.
“Kutokana na wingi wetu, tuliamua kuanzisha VICOBA na baada ya kuona mafanikio ni makubwa , tukahamia kwenye SACOSS na kwa namna tunavyokwenda ndoto yetu ni kwenda kuanzisha benki. Kikubwa ni kuendelea kushirikiana na kuhakikisha wote tunajiunga kwenye SACOSS ili kufikia lengo la kufungua benki,”amesema.
Kwa upande wake Katibu wa TAWCA Prisca Ndali amefafanua waliamua kuanzisha VICOBA ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wanachama wao kuwa na sehemu ya kutunza fedha na baada ya kuona ni nyingi walamua kuanzisha SACCOS na ndani ya miezi sita wakajikuta wamepata Sh.milioni 70.
“Kutokana na mafanikio ambayo tumeyapata, tukaamua sasa muelekeo wetu ni kuwa na benki yetu ya Wanawake Wahasibu.Kama tulianza na VICOBA na ndani ya muda mfupi tukawa na SACCOS, hivyo hivyo katika muda mfupi ujao unakwenda kuanzisha benki yetu na tukianzisha benki kuna faida nyingi ikiwemo ya kutoa ajira kwa wanawake wengine, katika mkutano wetu wa siku mbili tumezungumza namna ya kuwainua wanawake wengine, hivyo benki hii itasaidia kuwainua wengine,”amesema Ndali.
Amesisitiza kinachowapa matumaini ya kufanikisha lengo la kuwa na benki ni kwamba wamejipanga na wana kila kitu na hata benki itakapoanza hawatakuwa na tatizo katika kuiendesha na kuisimamia kwani wanao watalaamu waliobobea kwenye mambo ya fedha na uhasibu.
Ametumia nafasi hiyo kuendelea kuwahamasisha wana-TAWCA ambao hawajajiunga na SACCOS yao kujiunga kwani kadri wanavyoendelea kujitafakari ndivyo ambavyo wanajichelewesha kunufaika.”Katika benki tunaamini haitapita miaka miwili tutakuwa na benki tayari, hivyo ambao hamjajiunga na SACCOS huu ni wakati wenu , jazeni fomu.”