Mwandishi Wetu -Dar es salaam
MUSSA Aboud Jumbe ambaye ni mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe naye amechukua fomu ya kuomba kuwania urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kufanya idadi ya walioomba ridhaa hiyo kufikia 30.
Jumbe anakuwa mtoto wa tatu wa marais wastaafu waliojitokeza kuchukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar.
Wengine ni Dk. Hussein Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Dk. Ali Hassan Mwinyi na Balozi Ali Abeid Karume ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.
Hatua ya Jumbe kuchukua fomu hiyo ya urais jana baadhi wanaona ni kama imezidi kuufanya mchakato huo kuwa mgumu hasa kwa upande wa waliojitokeza ambao wana sifa kama zake.
Jumbe alikabidhiwa fomu hiyo jana katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui na Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Idara ya oganaizesheni Zanzibar.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, kada huyo aliwataka Wazanzibari kumwombea ili afanikiwe katika mchakato huo wa urais.
“Nafahamu kabla yangu, wako wengi waliofika kwa ajili ya kupata ridhaa ya chama na baada ya hapo kupata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar, nisingependa leo (jana) kuzungumza mengi sana, niwaombeni tu nanyi muwe pamoja nami.
“Mniunge mkono katika kuniombea kwa Mungu lililokuwa lenye kheri liweze kufikia pale inapostahiki, baada ya hayo nisingelipenda kuzungumza zaidi,”alisema Jumbe.
13 WARUDISHA FOMU
Wagombea waliorejesha fomu hizo za urais jana ni pamoja na Profesa Mbarawa, ambapo alisema anaishukuru CCM kwa kusimamia zoezi hilo vizuri.
“Nimekamilisha kujaza fomu na kutimiza yote niliyotakiwa kufanya na hakuna changamoto yoyote niliyoipata, CCM kina utaratibu mzuri tunashukuru uongozi kwa kusimamia jambo hili,”alisema Profesa Mbarawa.
Mgombea mwingine aliyerudisha fomu jana ni Shamsi Vuai Nahodha ambapo aliwashukuru wanachama wote waliomdhamini.
“Tumekwenda salama na kurudi salama, nawashukuru wote walionipa heshima kubwa ya kunidhamini,”alisema Nahodha.
Aliyehitimisha zoezi hilo la urejeshaji fomu jana ni Ayoub Mohammed Mahmoud, ambapo alisema kwa upande wake zoezi la wadhamini halikuwa gumu.
“Zoezi hili kwangu halikuwa ngumu hata kidogo isipokuwa changamoto ilikuwa ni wingi wa wadhamini lakini fomu zilikuwa chache na ziliwekwa kwa idadi maalumu,”alisema Mahmoud.
Makada wengine waliorejesha fomu kabla ya jana ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Balozi Ali Karume, Mohammed Hija Mohammed, Mbwana Bakari Juma, Abdulhalim Mohammed Ali na Hamis Mussa Omari.
Wakati zikiwa zimebaki siku tatu tu kwa zoezi la uchukuaji fomu na urejeshaji kufungwa, baada ya hapo wanachama waliotia nia watasubiri hatua inayofuata ya uchujaji ili kupata idhini ya kuingia katika mchakato wa kumrithi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, anayemaliza kipindi cha uongozi wake wa miaka 10 tangu achaguliwe mwaka 2010.
Tangu zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu, sambamba na utafutaji wadhamini lifunguliwe Juni 15 mwaka huu, takribani watu 30 wamejitosa katika mchakato huo, ambapo wanawake waliojitokeza hadi sasa ni watatu na wanaume 27.
Wanawake waliojitokeza ni Mwatum Mussa Sultan, Hasna Atai Masoud na Fatma Kombo Masoud.
Zoezi hilo linatarajiwa kufika tamati Juni 30 mwaka huu saa 10:00 jioni.
Wagombea wengine waliochukua fomu ni pamoja na Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha, Mohammed Jaffar Jumanne, Mohammed Hijja Mohammed, Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor na Profesa Makame Mnyaa Mbarawa.
Wengine ni Mwatum Mussa Sultan, Haji Rashid Pandu, Abdulhalim Mohammed Ali, Jecha Salum Jecha, Dk. Khalid Salum Mohammed, Rashid Ali Juma, Khamis Mussa Omar, Mmanga Mjengo Mjawiri, Hamad Yussuf Masauni, Mohammed Aboud, Bakar Rashid Bakari, Hussein Ibrahim Makungu, Ayoub Mohammed Mahmoud, Hashim Salum Hashim pamoja na Hasna Attai Masoud.
Juni 15 mwaka huu ndiyo ilikuwa siku ya kwanza ya uchukuaji fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi wa mwaka huu.
Waliofungua dimba ni mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Balozi Karume na Bakari Juma.
Pamoja na kuwa na wingi wa wagombea ambao wanavunja rekodi ya mwaka 2010 ambapo kulikuwa na wagombea 11 pekee waliokuwa wakitaka kumrithi Aman Abeid Karume, safari hii kumekuwa na mwamko mkubwa wa makada wa CCM kuomba nafasi ya uteuzi wa CCM ili kuwania urais wa Zanzibar.