Na Hamisa Maganga, Dar es Salaam
PENGO lililopo ni kubwa kati ya walionacho na wasionacho. Rais Dk. John Magufuli ametoa jina jipya – anawaita wanaoishi kama mashetani na wanaoishi kama malaika, kwa kweli wameachana mbali.
Rais Dk. Magufuli anamaanisha kuwa wenye kipato cha chini wamekuwa wakiishi kwa tabu wakati wale wenye kipato kikubwa hawajui kama kuna kitu kinaitwa shida.
Huwa naamini siku zote maisha waliyonayo wazazi wako ndiyo ambayo utakuja kuishi wewe baadaye, labda utokee muujiza. Hii ni kwa sababu walionacho huongezewa na wasionacho hubaki hapo walipo.
Sijui, labda siku moja Rais Dk. Magufuli atakuja kubadili nadharia hii, hatimaye Watanzania tukaishi tukiwa sawa au kupishana kwa kiwango kidogo.
Ukilinganisha mishahara ya vigogo hapa nchini na ya wafanyakazi wa kawaida, unaweza usitamani kuajiriwa. Pengo ni kubwa mno, tuombe Mungu hali ibadilike, viwango vya mishahara viboreshwe, kima cha chini angalau kikidhi mahitaji ya mfanyakazi.
Njozi ya kuongezwa mishahara
Wafanyakazi wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kilio chao cha kutaka kupandishwa kwa kima cha chini cha mishahara na kupunguza kiwango cha makato ya kodi kufanyiwa kazi na Rais Magufuli ili nao waondokane na maisha ya kishetani na kuishi kama malaika.
Siku moja kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi – Mei Mosi, Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Hezron Kaaya, alisema wafanyakazi wanategemea kima cha chini cha mshahara kitapanda hadi kufikia Sh 750,000 ili kuweka uwiano wa kipato na gharama za maisha.
Hata hivyo, akihutubia wafanyakazi katika sherehe za Mei Mosi mjini Dodoma wiki hii, Rais Magufuli alishindwa kumaliza kilio chao cha kutaka kuongezewa mishahara, badala yake akawaahidi kuwa atalifanyia kazi suala hilo wakati mwingine kwa kuwa hivi sasa amejielekeza katika mapambano dhidi ya wafanyakazi hewa.
Hata hivyo, Rais Magufuli hakuwaacha hivi hivi wafanyakazi, akawapunguzia machungu kwa kuwatangazia kupunguza kiwango cha makato ya kodi katika mishahara yao kutoka asilimia 11 ya awali hadi 9 kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017, kitu ambacho pia ni faraja kubwa kwao.
Kima cha chini cha mshahara
Katiba ya Tanzania inasema kila mtu ana haki ya kupata ujira kutokana na kazi anayoifanya, na wote wanaofanya kazi wanapaswa kupata stahiki zao za malipo kwa kadiri ya utendaji na sifa za kufanya kazi husika.
Kila mtu ana haki ya kupata malipo stahiki. Viwango hivi huwekwa na bodi za mishahara za kisekta ambazo zipo kwa mujibu wa Sheria ya kazi ya mwaka 2007.
Ili kufikia viwango vya chini vya mshahara, bodi za mishahara za kisekta huzingatia vigezo muhimu kama vile gharama za maisha, hali ya mishahara nchini, uzalishaji, uwezo wa waajiri kuendesha biashara zao vizuri, utekelezaji kazi wa shughuli za kibiashara za kati, ndogo na ndogo sana.
Vigezo vingine ni kama biashara mpya, gharama za kuishi, kupunguza umaskini, kiwango cha chini cha kujikimu, malipo, makubaliano na masharti ya ajira kwa waajiriwa wa sekta mbalimbali katika eneo la Jumuia ya Afrika Mashariki.
Kwa sasa kuna viwango vya chini vya mshahara kwa sekta za ujenzi, shule binafsi, nishati, viwanda na biashara, hoteli na huduma za majumbani, ulinzi binafsi, madini, afya, uvuvi, usafirishaji, mawasiliano, kilimo na nyinginezo.
Malipo ya kawaida
Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 hutofautisha kati ya ujira na mshahara wa kawaida. Ujira ni thamani kamili ya malipo yote, kipesa au kwa njia yoyote, anayolipwa mfanyakazi kutokana na ajira aliyonayo.
Mshahara wa kawaida humaanisha sehemu ya ujira wa mfanyakazi unaolipwa kulingana na kazi iliyofanya wakati wa saa za kawaida za kufanya kazi, lakini haijumuishi marupurupu.
Sheria hii husimamia malipo ya mishahara kwa wafanyakazi wa aina yoyote. Inasema; mishahara inaweza kuhesabiwa kwa saa, kila siku, kila wiki au kila mwezi.
Kuhusu kupunguza mshahara
Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 inasema kwa ujumla, mwajiri haruhusiwi kupunguza mishahara isipokuwa ikiwa inahitajika au imeruhusiwa chini ya sheria iliyoandikwa, makubaliano ya pamoja, uamuzi wa mshahara, agizo la mahakama au tuzo la maombi ya rufaa.
Kwamba punguzo linaweza pia kufanywa iwapo mfanyakazi ataridhia, kwa kuandika kuhusu deni au kumfidia mwajiri kwa hasara au uharibifu aliousababisha. Kiwango cha jumla cha punguzo lazima kisiwe zaidi ya robo nusu ya ujira wa mfanyakazi.
Mwajiri anastahili kutoa risiti za malipo kwa wafanyakazi wote pamoja na malipo ya fedha taslimu au cheki; au kumpa mfanyakazi katika bahasha iliyofungwa iwapo ni fedha taslimu.
Mishahara ya wafanyakazi wa kawaida
Hadi kufikia mwaka jana, wafanyakazi wa kawaida walikuwa wakilipwa mshahara wa Sh 315,000; wapo wanaopata zaidi ya kiasi hicho, lakini pia wengine wanapata chini ya hapo. Ongezeko hili la mshahara ambalo pia halitoshelezi, lilifanywa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, wakati alipokuwa madarakani.
Sasa basi, katika hali isiyo ya kawaida unaweza kukutana na mtu anafanya kazi ngumu serikalini kwa mshahara wa Sh 250,000 kwa mwezi. Fedha hiyo ni ndogo mno, hasa ukizingatia kuwa hali ya maisha imepanda maradufu.
Gharama za usafiri, chakula, malazi na nyinginezo ni kubwa ukilinganisha na kiwango cha mshahara kinacholipwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliwahi kukiri kuwa mishahara ya wafanyakzi wa kawaida haitoshi na sehemu nyingine za kazi mazingira ni magumu, lakini pamoja na changamoto hizo, wafanyakazi wamekuwa wakifanya kazi kwa tija na ubunifu.
Mishahara ya vigogo
Hebu tafakari, wakati wewe unalalamika mshahara mdogo wa Sh 300,000 kwa mwezi, kuna watu katika mashirika ya umma wanalipwa mishahara minono kiasi kwamba wanao uwezo wa kulisha ukoo wote wakiamua.
Utakuta mtu mmoja anapokea mshahara wa Sh milioni 36 kwa mwezi na wengine hufikia hadi kiwango cha Sh milioni 40.
Baadhi ya taasisi ambazo zinatajwa kuwa na wafanyakazi wenye mishahara minono ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
ambao hulipana hadi Sh milioni 24 kwa mwezi pamoja na
marupurupu, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sh milioni 36 na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Sh milioni 36.
Taasisi nyingine ni pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Sh milioni 36 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Nia ya Rais Magufuli ni kuhakikisha kima cha juu cha mshahara kwa mfanyakazi kinakuwa Sh milioni 15 na si zaidi ya hapo.
“Atakayeng’ang’ania kwamba lazima alipwe Sh milioni 40 aache kazi tuweke mtu mwingine,” alisema Rais Magufuli alipokuwa akizungumzia suala la wafanyakazi kulipwa mishahara mikubwa na wengine kupata Sh 300,000 kwa mwezi.
Rais anaonekana wazi kuguswa na jambo hili na kujikuta akiita mishahara ya ajabu inayopangwa na vigogo kwa kushirikiana na bodi ambazo wakati mwingine huhongwa fedha ili kupandisha mishahara.
Kutoka milioni 40/- hadi 15
Kwa kuwa ulipaji wa mishahara minono kwa vigogo ndio uliotengeneza tabaka kubwa la wenyenacho na wasionacho, Rais Magufuli amemua jambo la msingi ambalo linaweza kuleta heshima na utu kwa Watanzania.
Kitendo cha Rais Dk. Magufuli kuhakikisha anaweka uwiano wa mishahara kwa watendaji wa
taasisi hizo utaisaidia kwa kiasi kikubwa kuleta uwajibikaji
na usawa kwa watendaji.
Hata hivyo, ili kuonyesha kuwa alichokisema hakikuwa cha masihara, siku chache baada ya kutoa agizo la kupunguza mishahara mikubwa ya watendaji wa mashirika ya umma, Serikali kupitia Bodi ya Mishahara ilianza kazi ya kufanya marekebisho hayo.
Akizungumza na MTANZANIA siku chache mara baada ya agizo hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema mishahara ya watumishi hao itapunguzwa na kuwa yenye uwiano ndani ya miezi 15.
“Katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa, tunayo Bodi ya Mishahara yenye jukumu la kufanya mapitio, imeanza kazi hiyo ili kuhakikisha mishahara haipishani sana.
“Hatua ambazo tumeanza kuzitekeleza, tayari mamlaka zetu zimeanza kukutana kupitia Utumishi, Hazina na Msajili wa Hazina ili kuangalia namna ya kulitekeleza agizo hilo,” anasema Waziri Kairuki.
Ili kuonyesha kwamba watu wenye mishahara midogo hawatendewi haki, Kairuki anatoa mfano: “Unakuta mtumishi wa taasisi X kiwango chake cha elimu, uzoefu, ujuzi, muda wa kuingia kazini pamoja na kazi anayoifanya ni sawa na ya mtumishi wa taasisi Y, lakini unakuta mtumishi X analipwa mshahara mkubwa zaidi ya mara tano ya mtumishi Y jambo ambalo si haki katika utumishi.”
Wafanyakazi wa wanena
Masija Paul ambaye ni mfanyakazi wa serikalini anasema: “Hata mishahara ya vigogo ikipunguzwa, sijui kama sisi wafanyakazi wa kawaida tutapata kiwango ambacho angalau kitatuwezesha kumudu gharama za maisha.
“Sijui, siwezi kukata tamaa kwa kuwa muda bado… labda ipo siku na sisi tutaonekana kuwa watu katika watu.”
Naye Mwalimu Dyness Martin, ambaye hakupenda shule yake iandikwe gazetini anasema: “Tatizo Serikali yetu ni ya maigizo, walimu wakuu waliahidiwa kupewa posho kila mwezi kulingana na elimu uliyonayo. Iliahidi kuwa mwalimu mkuu mwenye Shahada anaweza kupata posho ya hadi Sh 300,000 kwa mwezi mbali na fedha ya elimu bure inayopitia kwenye akaunti ya shule.
“Posho hii ni kwa ajili ya kumuwezesha mwalimu kufanya mambo mbalimbali akiwa shuleni, lakini hadi sasa kimya na hatujui nini kinaendelea.”
Mwalimu Martin anasema kuwa nia ya Rais Magufuli ni kuweka uwiano sawa kwa Watanzania, akiwa makini atafanikiwa, lakini ahakikishe anafanya mambo kwa utulivu maana anaweza kujikuta akipoteza wafanyakazi muhimu, ambao mapato ya taasisi zao na utendaji kazi unaendana na mishahara wanayopata.