Na AMON MTEGA – SONGE
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amewaagiza polisi kuwahoji wafanyabiashara watatu wa vyakula mkoani humo kuhusu madai ya kuhifadhi vyakula kwenye maghala yasiyo na vibali na kuficha baadhi ya bidhaa kama mafuta ya kula.
Mndeme alitoa amri hiyo jana alipofanya msako kwenye baadhi ya maghala ya wafanyabiashara yanayohifadhi vyakula.
Alichukua hatua hiyo lengo likiwa ni kubaini walioficha mafuta ya kula pamoja na sukari kisha kutangaza kuwa vimeadimika kuviuza kwa gharama kubwa.
Wafanyabiashara wanaoshikiliwa na polisi ni Oska Ngao ambaye alikutwa kwenye ghala lake akiwa na mafuta ya kula ndoo 759 huku sehemu ya kuhifadhia ikidaiwa kuwa ni hatarishi kwa walaji.
Ilidaiwa kuwa eneo la kuhifadhia mafuta hayo kuna bidhaa nyingine yakiwamo majani ya chai.
Habari zinasema chumba hicho zamani kilikuwa kikitumika kama choo.
Wafanyabiashara wengine ni Narende Ledi ambaye ghala lake lilikutwa na ndoo 3,200 za mafuta ya kula na Sokorid Miliam ambaye ghala lake lilikuwa na ndoo za mafuta 600.
Wafanyabiashara hao walidai hawajazificha bidhaa hizo bali wamezihifadhi siku za karibuni huku wakiendelea kuwauzia walaji.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Ledi alisema ana vibali vyote na biashara yake ipo wazi na hajaficha bidhaa yoyote isipokuwa ghala analolitumia lilikuwa jengo la bohari ya serikali na hakujua kama ghala hilo linatakiwa kuwa na kibali cha kuhifadhia bidhaa.