Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Utafutaji masoko ya madini, kuongeza thamani madini na ushirikiano baina ya nchi na wawekezaji ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na washiriki wa mkutano wa sita wa kimataifa katika sekta ya madini Tanzania.
Mkutano huo ulioanza Novemba 19 hadi 21,2024 ulihudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,500 kutoka nchi mbalimbali za Afrika huku ukiwa na kaulimbiu isemayo ‘Uongezaji thamani madini kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii’.
Wakizungumza Novemba 21,2024 wakati wa kuhitimishwa kwa mkutano huo, baadhi ya washiriki wamependekeza mambo kadhaa kwa mustakabali wa kukuza sekta hiyo nchini.
Mchimbaji wa madini kutoka eneo la Kalole Kahama mkoani Shinyanga, Elia Lunguya, amependekeza kufanyika kwa sensa kwenye maeneo yote yanayochimbwa madini kubaini wachimbaji wadogo.
“Itungwe sheria na Serikali ifanye sensa kwenye maeneo yanayochimbwa madini ili kubaini wachimbaji wadogo kwa sababu watu wengine wanapewa leseni kama wachimbaji wakubwa halafu wanageuka kuwa wasimamizi, shughuli zote zinafanywa na wachimbaji wadogo…tunataka haki za mchimbaji mdogo na mwenye leseni zijulikane,” amesema Lunguya.
Mchimbaji wa Madini ya Tin kutoka Kyerwa Kagera, Renatus Kapila, amesema soko la madini hayo limeshuka kwani kumekuwa na mnunuzi mmoja ambaye anasuasua na kuishauri Serikali kuwatafutia masoko.
“Soko la madini ya Tin linashuka kila siku, kuna mnunuzi mmoja ambaye anasuasua, tunaomba Serikali irejeshe utaratibu wa kuiuzia Stamico (Shirika la Madini la Taifa) ili kusaidia kuleta ushindani. Tuna mizigo mingi imejaa stoo na hata ukipeleka sokoni anasema hana fedha,” amesema Kapila.
Kredo Mwinuka amependekeza Serikali isaidie vyuo vya kati na vyuo vya ufundi ili viwe na maabara na vifaa vya kutosha kusaidia wanafunzi waweze kupata ujuzi utakaosaidia katika sekta hiyo.
Dk. Dalali Kafumu, amesema; “Tunahitaji kuwa na ushirikiano baina ya nchi na kufanya kazi pamoja, kama hatufanyi kazi pamoja hatutaweza kuongeza uwekezaji nchini kwetu na kwenye mnyororo mzima katika sekta ya madini.
Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, amesema wizara itaendelea kuboresha taarifa za kijiolojia kuwezesha utafutaji wa kina wa madini kwa ajili ya migodi huku akiwahakikishia wawekezaji wa ndani na nje kuendelea kushirikiana nao kwa manufaa ya kukuza sekta hiyo.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema wanafikiria kujenga eneo maalumu kwa ajili ya kufanyia mikutano hiyo kutokana na idadi ya washiriki kuongezeka kila mwaka.
“Kila mwaka mkutano huu unazidi kuongeza idadi ya washiriki kutoka sehemu mbalimbali na barani Afrika kwa ujumla, kwa sababu mwaka huu idadi imekuwa kubwa matarajio ya baadaye ni kuwa nae neo maalumu la mikutano ya madini. Wakuu wa mikoa ambao wako tayari kutenga maeneo makubwa ya mikutano ya madini watumie fursa hii,” amesema Mavunde.
Akifunga mkutano huo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, amesisitiza kujengwa kwa viwanda vitakavyoongeza thamani madini hadi kufikia uzalishaji na utengenezaji wa vifaa mbalimbali.
“Tunampongeza Rais Samia kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, amedhamiria kuiendeleza sekta ya madini, ameonyesha kwa vitendo nia yake njema ya kushirikiana na wawekezaji wa ndani na nje katika kuendeleza sekta ya madini,” amesema Mgeni.