Na Mwandishi Wet, Dodoma
Shindano la kumsaka mrembo atakae wakilisha Mkoa wa Dodoma katika kinyang’anyiro cha Miss Tanzania mwaka huu limezinduliwa rasmi leo Jumatatu Mei 10, 2021.
Mchuano huo unatarajiwa kufanyika June 21, mwaka huu jijini Dodoma ambapo warembo zaidi ya 20 watashindana katika jukwaa moja kutwaa taji hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, mlezi wa shindano hilo Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Morogoro, Norah Mzeru amesema tasnia ya urembo inahitaji kuungwa mkono kwa kuwa imekuwa ikiibua vipaji vya wasichana
“Nikiwa kama Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Morogoro katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nawaomba wabunge wenzangu kuchangia tasnii ya urembo na mitindo kwani inatoa Ajira kwa mabinti zetu pamoja na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii hapa nchini,”anasema Norah Mzeru.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa NIKALEX LTD, Alexander Nikitas ambae ni mwandaaji wa mashindano hayo amesema hiyo ni fursa kwa mabinti wa mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi ili kushiriki mashindano haya ambayo yatawapa nafasi za kushiriki Miss Tanzania ambapo mshindi wa kwanza mpaka wa tatu ndiye atakayepata nafasi ya kushiriki Miss Kanda Kati.
“Mashindano haya yanayotarajia kufanyika Juni 21, mwaka huu yatahusisha Wilaya zote saba za Dodoma hivyo mabinti wote wanakaribishwa kushiriki mashindano kwa kuchukua fomu katika mitandao ya kijamii ukurasa za Miss Tanzania,”amesema Alexander Nikitas.
Pia, Alexander Nikitas amesema jamii itambue kuwa tasnia ya urembo na mitindo imekuwa chachu katika kuwajengea mabinti kuwa wana jamii wenye kutegemewa kwa kuanzisha kampeni za kusaidia na kuelimisha jamii katika sekta mbalimbali.