25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wajitosa mapambano dhidi ya malaria

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

UMOJA wa wabunge ambao wapo kwenye mapambano dhidi ya malaria na magonjwa yasiyopewa kipaumbele (Tanzania Parliamentary Against Malaria and Neglected Tropical Diseases – Tapama), wameanza utekelezaji wa mpango wa kusaidia na kuwezesha ushiriki wa wabunge kuongeza utashi wa kisiasa ili kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Mradi huo unadhamiria kujenga uwezo na kuimarisha ushiriki wa kisiasa na uwajibikaji unaotokana na kuhamasisha upatikanaji wa takwimu sahihi za malaria kuanzia ngazi za majimbo, halmashauri hadi taifa.

Akizungumzia mkakati huo, Mwenyekiti wa Tapama, Riziki Lulida, alisema kuwa wanaunga mkono jitihada za Serikali katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria na wagonjwa wa malaria nchini.

“Kama takwimu zinavyoonyesha, kiwango cha maambukizi kimepungua kwa zaidi ya nusu yaani kutoka asilimia 14.4 mnamo mwaka 2016 hadi asilimia 7.3  mwaka 2018.

“Mafanikio haya muhimu yamekuwa ni matokeo mazuri ya kuratibiwa vizuri na Serikali kwa kupitia Mpango wa Kudhibiti Malaria (NMCP) wa Serikali ya Tanzania.

“Ili kuzuia hali ya maambukizi ya malaria kuongezeka tena, zinahitajika hatua madhubuti kudhibiti ongezeko la maambukizi kwa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake, pia tunahitajika kuongeza rasilimali zaidi, kuongeza ushiriki wa wadau mbalimbali,” alisema Lulida.

Alisema wao kama wabunge wana jukumu kubwa katika kuunga mkono maono na malengo ya Serikali kuelekea kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa wa malaria kufika sifuri ifikapo mwaka 2030 hapa nchini.

Katibu wa Tapama, Dk. Raphael Chegeni, alisema mradi huo utasaidia kuendeleza programu ya Kadi ya Alma ya tathmini ya uwajibikaji na utendaji wa malaria kwa kuiweka katika mfumo mtandao.

Alisema kupitia mradi huo wabunge watapatiwa mafunzo ya jinsi ya kutumia Kadi ya Alma ya tathmini ya  uwajibikaji na utendaji wa malaria, kufanya mikutano ya mara kwa mara na wananchi wao.

“Mpango huu utalenga zaidi katika kusaidia utendaji wa haraka wa kupunguza maambukizi ya malaria katika mikoa minne yenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huo  ambayo ni Kigoma, Geita, Kagera, Lindi na Mtwara.

“Mradi huu utaiwezesha Tapama kuhusika zaidi katika utetezi na uhamasishaji kikanda, ikiwa ni pamoja na kuchukua jukumu katika maadhimisho ya Siku ya Malaria ya SADC Novemba, mwaka huu,” alisema Dk. Chegeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles