Na MWANDISHI WETU -DODOMA
BAADHI ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji, wamehofia gharama za nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kusema ni kubwa na haziwalengi wananchi wa kawaida.
Wamesema kwamba pamoja na NHC kueleza mara kwa mara, kwamba nyumba hizo zinauzwa kwa gharama nafuu, kauli zao haziwezi kukubaliwa kwa kuwa zinauzwa kwa bei kubwa ambazo mwananchi wa kawaida hawezi kuzimudu.
Wabunge hao walitoa kauli hizo jana, walipokuwa wakizungumza wakati wa ziara yao ya kutembelea ujenzi wa nyumba 300 unaoendelea katika eneo la Iyumbu, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), alisema kama NHC wanawalenga wananchi wa kawaida, wanatakiwa kuangalia uuzaji wa nyumba hizo ili wengi waweze kuzinunua.
“Mmekuwa mkisema mnauza nyumba kwa gharama nafuu, lakini ukweli ni kwamba nyumba zenu mnazouza kwa gharama ya shilingi milioni 50, 60 na nyingine milioni 99, haziwezi kununuliwa na wananchi wa kawaida.
“Kwa hiyo, nawaomba muangalie upya bei zenu na kama tatizo ni VAT mnayotozwa kupitia vifaa vya ujenzi, ielezeni Serikali ili iangalie namna ya kuondoa VAT hiyo,” alisema Mwakajoka.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM), alilalamikia bei za nyumba hizo na kusema zinauzwa kwa gharama kubwa tofauti na nyumba zinazojengwa na Taasisi ya Viguta inayojenga nyumba kama za NHC na kuziuza kwa bei nafuu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chambani, Yusuph Salim Hussein (CUF), alisema kama NHC wanajenga nyumba ili kuwauzia wananchi wa kawaida, lazima washushe bei na kuuza kama inavyouza Taasisi ya Viguta.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mali za NHC, Haikamen Mlekio, alisema katika eneo hilo la Iyumbu, wanatarajia kujenga nyumba 300 ingawa kwa sasa wameshajenga 151.
Kwa mujibu wa Mlekio, mradi huo ulianza Desemba mwaka jana na unatarajia kukamilika Desemba 4, mwaka huu.