NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van Pluijm, amenasa mbinu za wapinzani wao katika Kombe la Shirikisho Afrika, Etoile du Sahel ya Tunisia, wanazotumia kwenye michezo mbalimbali wanayocheza.
Moja ya michezo hiyo ni ile dhidi ya Benfica de Luanda ya Angola, waliyoitoa kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo kwa mabao 2-1, Pluijm amedai kuwa ameziona mbinu zao na amewapa maelekezo wachezaji wake namna ya kukabiliana nazo.
Yanga inatarajia kuvaana na Etoile kesho kwenye mchezo wa raundi ya pili wa michuano hiyo, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Pluijm aliliambia MTANZANIA kuwa, anaijua vizuri Etoile na ameisoma kwenye mechi ilizocheza dhidi ya Benfica na za Ligi Kuu ‘Ligue 1’, huku akitamba kuutumia vema uwanja wa nyumbani kwa kuwachapa Watunisia hao.
“Etoile ni timu nzuri na yenye uzoefu, nimeisoma kwenye video katika baadhi ya mechi zao, ikiwemo ile ya Benfica, najua ubora wao na nimeanza kuwapa maelekezo wachezaji wangu, ili kufanyia kazi kwenye mechi hizo,” alisema.
Mholanzi huyo alisema wapinzani wao ni wazuri kwenye mbinu, hivyo kikosi chake kitakuwa na kazi kubwa ya kufunga mabao nyumbani, huku wakiwa na kazi nyingine ya kuhakikisha hawafungwi bao lolote.
“Kama unavyojua tunacheza nyumbani na tunatakiwa kuwaonyesha burudani mashabiki wetu, hili sina wasiwasi nalo, hivi sasa kikosi changu kimeimarika na tunacheza soka zuri la kasi, pasi hivyo ni fursa kwa mashabiki kujaa kwa wingi uwanjani kutushangilia,” alisema.
Akizungumzia hali ya kikosi chake, Pluijm alisema: “Kikosi changu kipo vizuri, ila kuna mchezaji mmoja ambaye ni majeruhi (Salum Telela), ambaye kesho (leo) hadi keshokutwa (kesho) hali yake itakuwa vizuri kwa ajili ya mchezo huo.”
Yanga inakutana na Etoile ikiwa na kumbukumbu ya kuitoa FC Platinum ya Zimbabwe kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2, huku Watunisia hao wakiwatoa Benfica de Luanda.
Kiingilio buku tano tu
Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, alisema wamepanga viingilio vya aina nne kwa mchezo huo, kiingilio cha chini kitakuwa ni Sh 5,000, viti vya rangi ya machungwa Sh 10,000, Sh 20,000 (VIP C), Sh 30,000 (VIP B), huku VIP A kikiwa ni Sh 40,000.
“Tiketi zitauzwa kwenye vituo 11 vilivyozoeleka tulivyotumia kwenye mechi zetu zilizopita dhidi ya FC Platinum, BDF XI. Yanga sisi ndio wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, hivyo tunawaomba mashabiki kuweka kando itikadi zao za timu na kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono Yanga,” alisema.
Etoile yaja na watu 56
Etoile du Sahel imeshatua nchini saa 9 usiku wa leo kwa ndege maalumu ya kukodi ya Kampuni ya Nouvelair bj 4870, ikiwa na msafara wa watu 56, wakiwemo wachezaji 19 wa kikosi hicho.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tunisia (FTF), Krifa Jalel, ndiye mkuu wa msafara huo akiwa na Rais wa timu hiyo, Charefeddine Ridha pamoja na benchi la ufundi lenye watu 13, waandishi wa habari 12 na wanachama wao 10, ambao wote watafikia kwenye Hoteli ya Ledger Plaza, zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi.
Kikosi hicho cha Etoile kitakachofanya mazoezi leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, kinaundwa na wachezaji Aymen Mathlouthi, Aymen Ben Ayoub, Hamdi Nagguez, Ghazi Abderrazzak, Tej Marouene, Rami Bedoui, Zied Boughattas, Ammar Jemal, Saddam Ben Aziza, Mohamed Saied Nidhal, Mohamed Amine Ben Amor.
Wengine ni Franck Kom, Mehdi Saada, Alaya Brigui, Hamza Lahmar, Youssef Mouihbi, Alkhali Bangoura, Sofiane Moussa na Baghdad Bounedjah, ambaye ndiye kinara wa upachikaji mabao kwa timu hiyo akiwa na mabao 10 kwenye Ligi Kuu Tunisia ‘Ligue 1’.