Na Hafidh Kido,
YAPO mambo mengi ya kujadili katika kipindi hiki ambacho kila uchao mijadala mbalimbali inaibuliwa. Baadhi ya mijadala hiyo ipo inayolenga kuliweka Taifa katika hali ya usalama na mingine kukosoa namna nchi inavyoendeshwa.
Katika makala haya nitaangazia suala la baa la njaa na ukame ambalo kwa namna moja ama nyingine mjadala wake umetawala kila kona nchini. Ni mjadala uliogawa makundi ya kila aina, wenye vyama na wasio na vyama, wenye njaa na wasio na njaa. Wenye ukame na kunyauka mazao yao yakiwemo mahindi na wale wasiokumbwa na ukame.
Tukiri mjadala huo upo, serikalini, mitaani, vyombo vya habari, yaani kila mahali mambo mawili yanayoongelewa ni njaa na ukame. Wengine hawajui tofauti, lakini wanajielekeza kwenye suala moja tu; tuna njaa.
Januari 17, mwaka huu Serikali imesalimu amri na kutangaza kusambaza chakula tani milioni 1.5 katika maeneo yaliyokumbwa na ukame ambako wananchi hawana chakula cha kutosha. Hii ina maana moja tu, kuna uhaba wa chakula nchini mwetu katika maeneo fulani ya wananchi.
Wiki iliyopita nilipata kusema Tanzania hakuna njaa bali uhaba wa chakula upo. Tena katika baadhi ya maeneo hali si nzuri kabisa na watu wana shida ya chakula.
Yapo mambo ya kubishana na yapo yasiyohitaji kubishana. Miongoni mwa yasiyo ya kubishana ni suala la uhaba wa chakula miongoni mwa miji na wanajamii.
Hakuna watu wenye akili nyingi kama wanasiasa, hakuna watu wachokonozi kama wanasiasa. Wanasiasa ni kama mabondia. Mwanasiasa akiona umepasuka sehemu yenye kukupa maumivu, yeye anapiga tena hapohapo kuongezea zaidi.
Hawajafanya hivyo mara moja au mbili. Tunafahamu miaka mingi wanafanya hivyo kwa kila utawala. Hao ndio wanasiasa na desturi zao za kufanya kazi za maumivu na kuzodoa mamlaka husika.
Ndio maana Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, alimteua Edward Lowassa kuwa msaidizi wake yaani Waziri Mkuu. Ili wakati yeye (Rais) akipiga siasa dhidi ya wapinzani wake, huku Lowassa atumie mtulinga (nguvu) kushughulikia wakorofi katika masuala ya utendaji kazi serikalini.
Hata Mwalimu Julius Nyerere alipomteua Rashid Kawawa alitaka hayo hayo kama ya Kikwete. Wakati Kawawa anashughulikia watu wakorofi serikalini, yeye (Nyerere) apige siasa dhidi ya wakosoaji wake.
Na kuna baadhi ya mawaziri wakuu kipindi cha Nyerere waliteuliwa ili kumpa nafasi rais apige siasa mfano ni kipindi cha uwaziri mkuu wa Edward Moringe Sokoine.
Lakini Waziri Mkuu wa sasa, Kassim Majaliwa, hakutaka kubaki nyuma. Wakati bosi wake anatumia nguvu na yeye akawa anatumia nguvu vile vile, akitumbua na yeye anatumbua kama mkuu wake.
Hata rais alipokwepa hoja ya uhaba wa chakula Waziri Mkuu Majaliwa naye akawa upande wa bosi wake, hadi aliposhauriwa (sijui na nani), kuwa afanye kazi yake kwa sababu maghala ya chakula yapo chini yake.
Sababu ya uhaba wa chakula ni nini?
Msimu uliopita wa mavuno wakulima waliuza sana chakula hadi nje ya nchi. Hata Serikali haikujisumbua kununua chakula ikiamini inayo akiba ya kutosha kwenye maghala.
Ndio maana huwezi kusikia maeneo ya mjini hakuna chakula, kwa sababu wakulima daima ndio wanaokabiliwa na njaa kwa kuwa wanauza kila kitu na kusahau akiba yao.
Hivyo, alichotakiwa kufanya rais ni kuacha kubishana na wanasiasa kwa sababu wanamtega.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa na utaratibu wake wa kutafuta ‘waropokaji’ wa kuwajibu wanasiasa huku viongozi wakichapa kazi.
Tatizo mwenyekiti huyu mpya wa CCM ameondoa vitengo vingi vilivyokuwa vikiisaidia Serikali iliyo madarakani kupumua. Matokeo yake Rais Magufuli anafanya kazi ya kujibu kila linaloibuliwa iwe mitandaoni au magazetini.
Kinachotokea ni kuwajibu watu kama kina Tundu Lissu wa Chadema, Zitto Kabwe wa ACT-Wazalendo hata mchumi na kada wa Chadema, David Kafulila.
Mtazamo wangu ni wote hao si saizi ya kujibiwa na Rais au mwenyekiti wa chama bali makada ‘waropokaji’ wanaojua siasa.
0713 593 894