NA ASHA BANI-DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuruhusu  watu waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura kutumia vitambulisho vya uraia   na leseni ya udereva katika uchaguzi wa marudio kwa kata 43, viongozi wa vyama vya siasa wamepinga hatua hiyo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 26 mwaka huu, baada ya kutangazwa kuwa nafasi hizo ziko wazi.
Wakizungumza   na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana,  viongozi hao walisema   uamuzi huo ni ukiukwaji wa taratibu na maadili ya uchaguzi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF upande wa Maalim Seif, Julius Mtatiro, alisema  ni ukiukwaji wa taratibu na njama za wazi za kutaka kuisaidia dola na kuhakikisha CCM inashinda uchaguzi huo wa marudio.
“Kwa uzoefu wangu NEC wanapotoa matamko ya aina hiyo huwa tayari wamekwisha kuwasiliana na CCM na malori ya mamia na maelfu ya wapiuga kura wasio na sifa husafirishwa kwenda kupiga kura katika maeneo yenye uchaguzi.
“Kama NEC ikitekeleza mchakato huo kwa sasa hakutakuwa na uchaguzi.
“NEC walijua kuna kata zinahitaji kurudia uchaguzi, walishindwa vipi kupeleka mashine za kuandikisha wapiga kura kuhakiki wapiga kura kwenye kata hizo kwa usimamizi wa mawakala wa vyama vya siasa?  Ndo utagundua kuwa kwa sasa wanafanya njama   za kuharibu uchaguzi,’’ alisema Mtatiro.
Alihoji uamuzi huo wa NEC na namna ambayo haikuvishirikisha vyama vya siasa jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.
Mkurugenzi wa Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema kwao ni jambo jipya   ambalo NEC imelisema bila kuwashirikisha wadau wake.
‘Ni jipya na hatulielewi na halijawahi kufanyika nchini ndiyo mara ya kwanza.
“Miaka iliyopita tulizoea kuona wapiga kura wakitumia kujaza fomu namba 17 lakini sisi tuliwahi kushauri waliojiandikisha kwenye daftari na wenye picha waruhusiwe wakagoma.
“Na hilo lilikuwa la mwaka 2014 sasa ni 2017 ni miaka minne… kuna watu waliokuwa na miaka 12 sasa ni 17. wana haki ya kupiga kura, ilitakiwa wawe wamekwisha kuwaandikisha na wala siyo jambo kubwa.
“Watu walitakiwa kujiandikisha siyo jambo kubwa kiasi hicho na watendaji wapo, kwa nini NEC haikutaka kushirikisha wadau?
“Hapa ilipaswa wadau kushirikishwa na kushauriana badala ya kuzunguka na kutoa matamko kwenye vyombo vya habari,’’ alisema Mrema.
Naye  Mwenyekiti wa CHAUMA, Hashim Rungwe, alisema hakuna ubaya na wala siyo shida kama wanaona inafaa watu kutumia hati ya kusafiria,  leseni ya gari na kitambulisho cha ukaazi.
Alisema kwa kuwa wao ndiyo wasimamizi na wameona kuwa inafaa wataweza kuhakikisha vinatumika kwa usahihi basi wafanye hivyo.
“Hakuna shida kama wao wanaona kuwa ni sahihi basi watumie ili mradi uwepo   usimamizi mzuri ambao hauwezi kuvunja sheria na haki kwa mpiga kura,’’ alisema Rungwe.
Juzi, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima, alisema wapiga kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata 43 unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu.
Alisema   wapiga kura hao wataruhusiwa kutumia vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),  hati za kusafiria na leseni za udereva.