Na FREDRICK KATULANDA-MWANZA |
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameiagiza Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kuangalia uwezekano wa kukagua au kupima ubora wa vyakula vinavyoliwa kwenye sherehe au harusi ili kulinda afya za walaji.
Akizungumza na wafanyakazi wa Maabara ya TFDA Kanda ya Ziwa jijini Mwanza mapema wiki hii, Waziri Ummy, alisema ana mashaka na ubora wa vyakula hivyo kwa kuwa vipo baadhi vimekuwa vikiliwa vikiwa katika hali isiyoridhisha.
“Siku moja niliulizwa swali, hivi vyakula vya kwenye sherehe nani anaangalia ubora wake, aliyeniuliza alieleza kuwa vinasafirishwa umbali mrefu na huko vitokako hatujui vinaandaliwaje, nani anafuatilia vinavyoandaliwa,” alieleza.
Alisema lengo la TFDA ni kulinda usalama wa walaji hivyo anadhani ipo haja ya kufuatilia kujua vinaandaliwaje na kubebwa katika mazingira gani mpaka kufika kwa walaji huku akibainisha yeye binafsi amewahi kula chakula kilichopoa harusini.
“Hapa simaanishi TFDA mwende kuharibu biashara za watu, lakini nadhani mkishirikiana na Idara ya Afya mnaweza kuja na mapendekezo yenu kwangu ya kuwa na namna bora ya kusimamia jambo hili ili tujiridhishe usalama wa vyakula hivi,” alisisitiza.
Alisema jukumu la TFDA ni kusimamia ubora hivyo ni vyema kuangalia namna ya kusimamia waandaaji vyakula hivi ikiwezekana kuweka utaratibu mzuri wa usalama kwa waandaaji na watoaji huduma za vyakula hata ikiwezekana kuwa na vifaa maalumu vya kusafirishia au vifungashio itakavyolinda ubora.
“Sijui nikisema haya kama mnanielewa, kuna familia moja walikula chakula harusini na wote walilazwa hospitali, sasa hiki chakula kilikuwa na shida gani au nani anajua ubora wake,” alieleza.
Hata hivyo, Waziri Ummy alitaka TFDA kufanya kazi zao kwa weledi ikiwa ni pamoja na kuitumia maabara hiyo kikamilifu kuleta ufanisi na kuhakikisha wanatoa huduma haraka na kuepuka kugeuka kikwazo cha wafanyabiashara kwa kuwaelekeza namna inayotakiwa.
Awali akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Agnes Kijo, alisema kujengwa kwa maabara ya kisasa ya Kanda ya Ziwa iliyopo Mwanza kumesaidia kudhibiti bidhaa zisizo na ubora.
Alisema kuwepo kwa maabara hiyo kumesaidia kupunguza kwa asilimia kubwa bidhaa zisizofaa ikiwa ni pamoja na dawa zilizopita muda wake japo alibainisha kuwepo kwa changamoto katika maeneo ya mipaka.
“Ofisi yetu ya Kanda ya Ziwa ilianza mwaka 2005 ikiwa na watumishi wawili na sasa wapo 36, imekuwa ikihudumia mikoa sita ya Kanda, hapa nieleze eneo hili lilikuwa likiongoza kwa dawa bandia na zisizo na ubora,” alisema.