Na HARRIETH MANDARI
VIWANDA vya kuchambua pamba vimezidi kupungua katika mikoa ya Kanda ya Ziwa licha ya wadau wa zao hilo kuzidi kusisitiza kilimo cha mkataba cha zao hilo.
Vilevile, bado tatizo la mbegu zisizokuwa na ubora limezidi kuchangia kusuasua kilimo cha zao hilo.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Bodi ya Pamba mkoa wa Geita, Gabriel Mwalo, amesema kilimo cha mkataba kimeanza kupokelewa vizuri na wakulima wa zao hilo kikitajwa kuwa suluhisho la uzalishaji mdogo wa zao hilo.
Mwalo alikuwa akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa zao hilo na Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, mkoani Geita hivi karibunii.
Alisema kilimo cha mkataba ambacho wakulima hupatiwa pembejeo kwa mkopo na kuzirejesha wanapovuna kimesaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kuwa wakulima wengi bado hawana uwezo kwa kununua pembejeo za kutosha.
Mkurugenzi alieleza kwamba wadau wa pamba mkoani Geita wameupokea kwa mikono miwili mpango huo kwa vile utahamasisha na kuinua uzalishaji wa zao lenyewe.
“Mpango wa kilimo cha mkataba ulianza msimu wa mwaka 2012/13 ambako uzalishaji ulikuwa tani 250,000 lakini baada ya mpango huo kuondolewa uzalishaji ulishuka hadi kufikia tani 225,000.
“Idadi ya viwanda vya kuchambua pamba vimepungua kwa sasa ambako mwaka 2015 vilikuwa viwanda 43 lakini hadi kufikia mwaka huu idadi imeshuka na kufikia viwanda 13 kutokana na wakulima kulima kwa kiasi kidogo,” alisema Mwalo.
Alisema bodi imekuwa ikipigia debe kilimo cha mkataba ili kurudisha hadhi ya kilimo hicho kwa kuwawezesha wakulima kuwa na uwezo wa kununua pembejeo za kisasa kuondokana na mavuno hafifu yanayosababisha viwanda kukosa malighafi na hatimaye kufungwa kuepuka hasara.
Naye Waziri Dk. Tizeba aliwaagiza wakurugenzi na watendaji wote wa halmashauri za mkoa huo kuhakikisha katika msimu huu wa kilimo kwa pamba, wakulima wanasambaziwa mbegu bora kuepuka urasimu wa upatikanaji wa mbegu hizo ambao ni changamoto kubwa katika uzalishaji.
“Serikali tayari imejipanga katika msimu wa 2017/18 kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa wingi.
“Tunawataka wasambazaji na mawakala wote wa pembejeo kila mmoja kwa nafasi yake kushiriki kufanikisha kilimo cha zao hilo ili kiwe na tija,” alisema Dk. Tizeba.