Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema jumla ya viwanda vipya 3,300 vimesajiliwa na mamlaka mbalimbali tangu Serikali ya awamu ya tano ingie madarakani, ambapo kati ya hivyo 652 ni vikubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi alisema ujenzi na uzalishaji wa viwanda hivyo uko katika hatua mbalimbali.
“Viwanda 250 vilisajiliwa kupitia kwa msajili wa makampuni, 361 vilisajiliwa na kituo cha ewekezaji, 41 vilisajiliwa na mamlaka ya usimamizi wa maeneo maalumu ya kiuchumi na 2721 vilisajiliwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO),” alisema Dk. Abbasi.
Alisema pia Kampuni Hodhi ya Raslimali za Reli (Rahco) tayari imetangaza zabuni ya kununua vichwa vya treni 25, ambapo kati yake 23 vitatumia nishati ya umeme huku viwili vikitumia diesel.
“Zabuni ya ununuzi wa mabehewa 1590 na mashine 25 za kukarabati reli ambapo kati ya mabehewa hayo 1,530 yatakuwa ni ya mizigo na 60 yakiwa ya kubeba abiria.
Akizungumzia kuhusu usafiri wa majini, Dk. Abbasi alisema tayari meli mbili mpya zimeanza kufanya kazi wiki iliyopita katika Ziwa Nyasa.
“Meli mbili mpya za mizigo ambazo ni Mv Njombe na Mv Ruvuma zinazobeba mizigo tani 1,000 kila moja zimeanza safari katika bandari mbalimbali zikiwamo za nje ya nchi,” alisema Dk Abbas.
Aidha Dk. Abbas alisema upande wa nishati ya umeme miradi ya Kinyerezi I Nyongeza umekamilika kwa asilimia 50 huku Kinyerezi II umekamilika kwa asilimia 87 na yote itachangia Megawatti 425 katika gridu ya taifa.
Dk. Abbasi pia alizungumzia safari ya serikali kuhamia Dodoma ambapo alisema jumla ya wafanyakazi 3,617 kutoka wizara na sekta mbalimbali za serikali wamehamia makao makuu hayo.
“Kwa mwaka huu tunatarajia wafanyakazi wengine 2,460 watafuata katika awamu hii hivyo niiombe sekta binafsi kuchangamkia kupeleka huduma huko,” alisema Dk. Abbasi
Kwa upande wa uchumi alisema kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IFM), Benki ya Dunia na Taasisi ya Goldman Sachs ya Marekani uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 6.8.
“Kwa sasa Tanzania inashika nafasi tano za juu katika ukuaji wa uchumi barani Afrika ikiongozwa na Ethiopia(aslimia 8), Ivory Coast (7.3), Senegal (7) na Tanzania ikiwa nafasi ya nne (6.8),” alisema Dk Abbas.