32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

VITA YA TRUMP NA VYOMBO VYA HABARI YAFIKA PABAYA

Rais Donald Trump akiwa katika moja ya mikutano na wanahabari

WASHINGTON, MAREKANI

KANA kwamba imekuwa hadithi ya kubuni juu ya uhusiano kati ya rais wa nchi na wananchi wake wa taifa la kusadikika.

Lakini kwa wananchi wa Marekani, imekuwa hali halisi ambayo wanaishuhudia kila siku, kwani Rais wao Donald Trump hana uhusiano mzuri na baadhi ya vyombo vya habari tangu kipindi cha kampeni za urais hadi pale alipotangazwa kuwa mshindi dhidi ya Hilary Clinton.

Ilitarajiwa uhasama kati ya vyombo vya habari vya Marekani na Rais Trump ungelikoma pale matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa, lakini haikuwa hivyo.

Vita kati ya Trump na waandishi wa habari inaelekea kuota mizizi licha ya kujitanabaisha kuwa rais wa wananchi wote bila kubagua nafasi na nasaba zao.

Hali ya kushamiri vita hiyo imejidhihirisha kwa mara nyingine tena, baada ya awali kuwakejeli waandishi wa shirika la habari la CNN, ikiwamo kumtimua mmoja wa waandishi waliouliza swali katika mkutano wake na wanahabari.

Juzi, Ikulu ya Rais wa Marekani ya White House imeyazuia mashirika kadhaa makuu ya habari kuhudhuria kikao cha wanahabari kilichoendeshwa na msemaji wa Ikulu, Sean Spicer.

Wanahabari wa CNN, The New York Times, Politico, Los Angeles Times na BuzzFeed hawakuruhusiwa kuhudhuria kikao hicho.

Utawala wa Rais Trump umekuwa ukiyashutumu mashirika hayo kuwa yanaeneza habari za uongo na za kupotosha.

Spicer hakutoa maelezo kwanini waandishi wa habari wa mashirika hayo waliachwa nje ya kikao kisicho rasmi cha wanahabari, hatua ambayo imeibua shutuma kali.

Shirika la habari la Reuters pamoja na mashirika mengine 10 yakiwamo Bloomberg na CBS, yaliruhusiwa kuhudhuria mkutano huo.

Wakati wanahabari kutoka CNN na mashirika mengine yaliyoathiriwa yalipojaribu kuingia Ikulu, yalizuiwa kwa kuambiwa majina yao hayako katika orodha ya wanahabari walioalikwa.

 

WANAHABARI ADUI

Katika mkutano wa wanaharakati wa kisiasa wa jumuiya ya wahafidhina ya CPAC, Rais Trump alivishutumu baadhi ya vyombo vya habari ambavyo anadai vinatoa taarifa za uongo na kuvitaja kuwa adui wa watu wa Marekani.

Spicer alisema kundi lake liliamua kufanya mkutano mdogo wa wanahabari katika ofisi yake badala ya mkutano rasmi kama ilivyo desturi katika chumba cha wanahabari katika Ikulu ya Rais akisema hawahitaji kuendesha kila kitu mbele ya kamera kila siku.

Wanahabari kutoka mashirika ya Associated Press (AP) na Jarida la Time waliondoka katika kikao hicho walipoarifiwa kuwa wanahabari wenzao kutoka mashirika mengine wamezuiwa kuhudhuria kikao hicho.

Taarifa kutoka kwa mhariri mkuu wa The New York Times, Dean Baquet imesema jambo kama hilo halijawahi kutokea katika Ikulu ya Rais ya White House katika historia yao ndefu ya kuripoti taarifa kutoka tawala chungu nzima kutoka vyama tofauti vya kisiasa nchini Marekani.

Baquet alisema wanapinga vikali kuzuiwa kwa gazeti lao na mashirika mengine ya habari na kuongeza kuruhusiwa kwa vyombo hivyo kuwa na uhuru na kuangazia matukio ya Serikali iliyo wazi bila shaka ni muhimu kwa masilahi ya taifa.

Chama cha Waandishi wa Habari za Ikulu ya White House (WHCA) pia kimepinga hatua hiyo ya Spicer.

Rais wa chama hicho, Jeff Mason ambaye ni ripota wa Reuters, alisema wanapinga vikali jinsi kikao kilivyoendeshwa na Ikulu ya White House.

 

TRUMP NA WANAHABARI

Katika kipindi cha kampeni mwaka jana, kundi la Trump liliyapiga marufuku mashirika kadhaa likiwamo gazeti la Washington Post na Buzzfeed dhidi ya kuripoti katika mikutano ya kampeni likiyashutumu kwa upotoshaji na kueneza habari za uongo.

CNN iliandika katika ukurasa wake wa Twitter ikisema kitendo cha kuzuiwa kwa baadhi ya mashirika ya habari si jambo linalokubalika kutoka kwa utawala wa Trump na huenda ndivyo Ikulu ya rais inavyojiendesha wakati taarifa za kweli ambazo hawazipendi zinaporipotiwa.

Katika hatua nyingine, CNN imeapa kuendelea kuripoti licha ya hatua kandamizi kama hizo.

 Mhariri wa BuzzFeed, Ben Smith pia ameishutumu Ikulu ya Rais Trump kwa kuyaadhibu mashirika ambayo yanaandika taarifa ambazo hawapendi ziandikwe na kuendelea kusema hawatasita kuripoti kuhusu utawala huo mpya kwa njia iliyo huru na ya haki.

Spicer alisema Ikulu ya Marekani inapanga kupambana dhidi ya kile alichokitaja kuangaziwa kionevu na vyombo vya habari.

 Msemaji huyo wa Ikulu alieleza kuwa hawatakaa tu na kuruhusu taarifa za uongo na za kupotosha zikitolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles