29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Vita ufisadi kupangua zaidi baraza la mawaziri

ISIJI DOMINIC

MWISHONI mwa Januari mwaka huu, msafara wa Rais Uhuru Kenyatta ukiwa njiani kuelekea Arusha kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa Afrika Mashariki ulisimamishwa na wananchi waliofurika maeneo ya Kitengela na kumtaka awahutubie.

Rais Uhuru aliitikia wito huo ikiwa ni muda mchache baada ya kufanya kikao cha baraza la mawaziri uliohudhuriwa pia na Naibu Rais William Ruto. Rais alibainisha kuwa aliwaambia mawaziri wake wanaotaka kupiga siasa wakae pembeni ili atoe kazi kwa vijana wengine ambao wapo wengi.

Ni kauli ambayo wachambuzi wa siasa walisema inawalenga mawaziri ambao muda mwingi wamekuwa wakimpigia debe Naibu Rais Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. Hata hivyo, Ruto baadaye alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akiwakana wale wanaoandamana naye kufungua miradi ya maendeleo na baadaye kuanza kupiga siasa.

Kwa siku za hivi karibuni, Serikali imegonga vichwa vya habari nchini Kenya kwa kashfa za ufisadi ikiwahusisha mawaziri na inadaiwa Rais Uhuru ameghadhabishwa hivyo kuanza kusuka mpango wa kufanya mabadiliko makubwa katika baraza la mawaziri.

Aidha inadaiwa Rais Uhuru amekasirishwa na watu wake wa karibu aliowaamini kuwatumikia wananchi kuhusishwa na kashfa za ufisadi na amepanga kuwaambia mawaziri wote wanaotuhumiwa kuachia ngazi au watimuliwe. Tayari wiki iliyopita Waziri wa Michezo, Rashid Echesa, alifungashiwa virago na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Balozi Amina Mohammed. 

Lakini ni vita dhidi ya ufisadi ambayo Rais Uhuru anapambana nayo na amewapa onyo kali mawaziri kwamba hatawavumilia. Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi ya Makosa ya Jinai (DCI) inawachunguza mawaziri wawili kutokana na matumizi mabaya ya takribani Sh.bilioni 486 ambayo ilitengwa kwa ujenzi wa mradi wa mabwawa.

DCI George Kanoti anawachunguza viongozi wote wa Serikali ikiwamo mawaziri hao kuhusu upotevu wa fedha hizo zilizokusudiwa kutengeneza mabwawa ya Arror na Kamwarer yaliyopo kaunti ya Elgeyo Marakwet. Mawaziri hao wawili huenda wakakabiliwa na makosa ya uzembe au kushiriki kuiba fedha za umma. Inadaiwa Rais Uhuru amemwagiza DCI kuharakisha upelelezi huo.

Imeelezwa pia polisi wamepata picha za CCTV kutoka hoteli ambayo ofisa mmoja mkubwa wa serikali alifikia akiwa nje ya nchi na inaonesha akikutana na kupokea fedha taslimu kwa wawakilishi wa kampuni iliyopewa zabuni kutengeneza mabwawa hayo. Ofisa huyo na timu yake walirudi Nairobi na fedha hizo ambazo zimehifadhiwa kwenye shimo katika nyumba ya kifahari.

Huku polisi bado wakiendelea na uchunguzi, Rais Uhuru ameombwa kuwatimua kazi mawaziri wanaohusishwa na ufisadi. Kinara wa upinzani, Raila Odinga na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi, Francis Atwoli, wanawataka maofisa wanaotuhumiwa kukaa pembeni ili kupisha uchunguzi.

“Adui wa Serikali si vyama vya wafanyakazi ila wale wanaohusishwa kuiba fedha za walipa kodi. Wanachohitaji wafanyakazi ni vyama vyao kutetea maslahi yao,” alisema Raila wakati akihutubia mkutano wa 30 wa vyama vya wafanyakazi chini ya Pan-African.

Macho yote sasa yapo kwa Rais Uhuru ni hatua gani atakayochukua katika kuboresha baraza la mawaziri. Lakini wanachokitaka wananchi ni kuona taasisi zote za serikali zinazopambana na rushwa hususani DCI akiwafikisha mahakamani mawaziri waliohusika na upotevu wa fedha za umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles