26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

VIONGOZI KUWENI MAKINI NA KAULI ZENU 


Yupo mtu mmoja anaitwa Phil Owens ambaye alipata kuandika kupitia moja ya safu muhimu inayopatikana kupitia tovuti ya Forbes kuhusiana na uongozi.

Katika andiko lake hilo la uongozi, Phil anasema kauli anayotoa kiongozi ina umuhimu, namna anavyozungumza, taarifa au usahihi wa kile anachokizungumza na zaidi nidhamu yake ni jambo muhimu sana.

Phil anasema haijalishi namna unavyopambana kujaribu kama kiongozi, watu lazima watatafsiri kila kitu unachokisema au kukifanya kama kiongozi kupitia lensi zao wenyewe na uzoefu wao.

Anasema viongozi wanapofanya bidii ya kuwasiliana kwa hata jambo moja, bado watu watanyambua na kupata maana yao, wakati mwingine kwa namna ya kupotosha kabisa kuliko vile ulivyomaanisha.

Anasema hata kama kiongozi akiamua kuacha kuzungumza lolote, kuna wakati watu wanaweza kutafsiri ukimya wako kwa namna fulani.

Phil anasema viongozi wanatakiwa kutambua kuwa wanawasiliana wakati wowote na kila mtu, ndani au nje ya uongozi wao, haijalishi kile wanachokisema au wanachokifanya.

Tumelazimika kukumbuka andiko hilo la Phil kutokana na kauli aliyoitoa wiki hii Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kuhusiana na majibu aliyoyatoa bungeni kuhusiana na tuhuma za wananchi wanaouawa wakiwa katika mikono ya polisi.

Lugola ambaye alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji, aliyehoji mkakati wa Serikali kukomesha matukio ya mahabusu wanaodaiwa kufariki dunia wakiwa mikononi mwa polisi alisema suala la mtu kufa halichagui mahali anapotakiwa kufia kwani kifo ni mtego.

Akifafanua kauli yake, Lugola alikwenda mbali na kusema kifo ni ahadi ya Mungu na mtu anaweza kufariki mahali popote.

Kwetu sisi tunaona hii ni kauli ambayo haikupaswa kutolewa na mtu anayeitwa kiongozi.

Kwetu sisi tunaona Lugola kama kiongozi aliacha kujibu hoja ya msingi na kupiga porojo na hivyo kukiuka misingi ya uongozi.

Tuhuma za watu kufia mikononi mwa polisi ni nyingi, lakini pia Lugola amejibu swali akisahau kwamba upo ushahidi wa kutosha wa polisi kushambulia raia kwa vipigo vikali.

Lugola amejibu swali hilo akisahau kwamba upo ushahidi wa kutosha wa polisi kutumia nguvu nyingi mahali ambako hawatakiwi kufanya hivyo.

Kauli ya Lugola kama kiongozi ilitakiwa kutoa njia na kutatua tatizo ambalo baadhi wameliona na hata kutaka majibu ya msingi.

Pengine kwa sababu ya nafasi tu, Lugola na viongozi wengine wanapaswa kutenda na kuiishi misingi ya uongozi kama andiko la Phil linavyoeleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles