Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewafikisha mahakamani wakurugenzi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa tuhuma za uhujumu uchumi.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wao, ubadhilifu, ufujaji na kusababisha hasara.
Takukuru iliwafikisha watuhumiwa hao Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na walisomewa mashtaka na wakili wa taasisi hiyo, Emmanuel Jacob.
Jacob aliwataja washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri kuwa ni Mkurugenzi wa Elimu, Baraka Issa, Mhasibu, Emmanuel Mayuma, Naibu Mkurugenzi wa Elimu, Hellen Lihawa na Mhasibu Msaidizi, Mbarouk Dachi.
Alidai kuwa Julai 16, mwaka 2014 katika ofisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo kwa sasa ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, washtakiwa hao wakiwa waajiriwa wa wizara hiyo, walitumia nyaraka za uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri wao.
Alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao kwa nafasi walizokuwa nazo, kwa lengo la kumdanganya mwajiri wao, walitumia hati ya malipo ya Julai 16, mwaka huo yenye jina la Emmanuel Mayuma, iliyokuwa na maelezo ya uongo, wakionesha kiasi cha Sh 18,411,000 kilitumika kwa malipo ya washiriki wa mafunzo ya michezo yaliyofadhiliwa na British Council Dar es Salaam wakati wakijua si kweli.
Katika shtaka la pili, Jacob alidai kuwa kati ya Julai 16 na Septemba 30 mwaka 2014 katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, washtakiwa hao kwa pamoja walitumia nafasi walizokuwa nazo kufanya ubadhilifu na ufujaji wa Sh 18,411,000 fedha ambazo zilikuwa za mpango wa kufadhili mafunzo kwa walimu wasiobobea wa shule za msingi katika kutoa huduma ya matumizi ya kadi za michezo Dar es Salaam.
Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa katika shtaka la tatu, kati ya Agosti 10 na Septemba 30, 2014, Mhasibu Emmanuel Mayuma alifanya ubadhilifu na ufujaji wa Sh 31,717,000 fedha ambayo ilikuwa ya mafunzo kwa walimu wa michezo katika matumizi ya kadi za michezo Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika shtaka la nne, Mayuma anadaiwa kuwa katika kipindi hicho cha kati ya Agosti 10 na Septemba 30, 2014 alifanya ubadhilifu na ufujaji wa Sh 7,000,000, katika shtaka la tano alifanya ubadhilifu na ufujaji wa Sh 2,500,000 fedha ambazo zilikuwa za mafunzo katika matumizi ya kadi za michezo Mkoa wa Dar es Salaam na zote zilikuwa ni ufadhili wa British Council.
Katika shtaka la sita washtakiwa wote wanadaiwa kuwa Julai 16 mwaka huo waliisababishia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hasara ya Sh 18,411,000 kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Kwa upande wa shtaka la saba, mshtakiwa Mayuma anadaiwa kuwa kwa makusudi aliisababishia wizara hiyo hasara ya Sh 41,217,000.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi haujakamilika.
Washtakiwa wametakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na kila mmoja asaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 90, wawe na vitambulisho na washtakiwa wasitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Kesi hiyo iliyosikilizwa na kutolewa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha kibali cha kuipa mamlaka ya kuisikiliza, imeahirishwa hadi Machi mosi mwaka huu.