Mwandishi Wetu
HATUA ya CCM kumwondoa ndani ya chama hicho, Bernard Membe sasa inakumbusha hadithi ya orodha ndefu ya makada wengine waliowahi kukumbwa na kadhia kama hiyo.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1985 CCM iliwatimua Maalim Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid Mohamed, Juma Duni Haji kwa tuhuma za kukihujumu chama hicho katika uchaguzi huo baada ya kutoridhika na uamuzi wa CCM kumpitisha Abdul Wakili, kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar.
Makada hao wote baadae walijiunga na chama cha upinzani cha CUF na kutikisa chaguzi kuu zote visiwani humo tangu mwaka 1995 baada ya kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Maalim Seif ameongoza harakati za upinzani akiwa na vigogo wenzake hao kupitia CUF kabla ya kuzuka kwa mgogoro wa kiuongozi ndani ya chama hicho ulichowalazimisha kukihama na kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo.
Mbali na vigogo hao, mwaka 2017 chama hicho kilimtimua aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Sophia Simba kwa kukihujumu chama katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Hata hivyo Sophia alirejeshwa ndani ya CCM baada ya kuomba msamaha na tangu wakati huo amekuwa kimya.
Pia chama hicho kiliwatimua wenyeviti wa mikoa mbalimbali akiwamo Ramadhan Madabida (Dar es Salaam), Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya (Mara) na wajumbe wa NEC, Ali Sumaye, Mathias Manga (Arumeru).
Wengine waliong’olewa katika sekeseke hilo ni pamoja na wenyeviti wa chama wilaya Madenge (Kinondoni), Assa Simba (Ilala), Leiza (Longido), Saileli Mollel (Arusha Mjini) Omary Hawadhi (Gairo) wenyeviti wa wilaya za Muleba, Babati na Bunda.